MAVUNDE AZINDUA JENGO LA KUPUMZIKA NDUGU WA WAGONJWA
Na. Wellu Mtaki, Dodoma
Mbunge wa Dodoma Mjini na Waziri wa Madini, Anthony Mavunde amezindua jengo la kupumzikia ndugu wa wagonjwa wanaopatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma.
Uzinduzi huo umefanyika juni 25,2025 huku akionyesha furaha yake baada ya kutimiza ahadi na ndoto ya muda mrefu tangu Mwaka 2010 akiwa mgombea ubunge kwa mara ya kwanza.
Mavunde ameeleza kuwa kumbukizi ya tukio ya siku moja alipofika hospitalini akiwa ameambatana na mgonjwa wakati wa usiku alikuta wananchi wamelala nje ya geti wakichanganyika bila kujali jinsia hali ambayo alishikwa huruma ya kuwa na haja ya kujenga jengo ilo ambalo Jengo hilo lina mabenchi 24 ya kukalia, televisheni kwa ajili ya kutoa taarifa muhimu na uzio kwa ajili ya usalama.
Aidha amesema kuwa Mwaka 2017 alianzisha mfumo wa kidijitali kuhakikisha kuwa watumishi wanafika kazini kwa wakati na kuwahudumia wagonjwa kwa heshima.
Pia ameeleza kuwa alifunga kamera na maikrofoni katika eneo la huduma za wagonjwa wa nje ili kuimarisha uwajibikaji na kuhakikisha wagonjwa wanapata huduma bora.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Rosemery Senyamule ambaye alikuwa mgeni rasmi katika uzinduzi huo amesema jengo hilo ni tumaini jipya kwa wananchi na litaleta faraja kwa wale wanaouguza ndugu zao hospitalini huku alimpongeza Mavunde kwa moyo wake wa huruma na kwa kutimiza kwa vitendo ahadi alizozitoa
Naye Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma Dkt Ibenzi Ernest amesema kuwa dira ya hospitali hiyo ni kutoa huduma bora kwa wananchi na kwamba mchango wa Mbunge Mavunde umekuwa wa thamani kubwa kwa maendeleo ya hospitali hiyo.
Alisema licha ya changamoto mbalimbali ikiwemo uhaba wa watumishi na uzio wa hospitali bado hatua kama hizi zinaonyesha jitihada za kweli katika kuboresha huduma kwa wananchi wa Dodoma na wageni wanaofika kutibiwa.

