Breaking News

Chuo cha NIT Kuimarisha Mafunzo ya Marubani na Kuboresha Usafirishaji: Hatua Muhimu kwa Maendeleo ya Tanzania

 







Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam

Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) kinakaribia kupata cheti kitakachowawezesha kutoa mafunzo ya marubani kwa viwango vya kimataifa, hatua ambayo inatarajiwa kubadilisha taswira ya sekta ya usafiri wa anga nchini Tanzania. Hii ni sehemu ya juhudi za serikali kuboresha miundombinu ya usafiri wa anga na majini, ili kuimarisha uchumi na biashara za kikanda.

Katika Mkutano wa Pili wa Kimataifa wa Usafiri, Usafirishaji, na Usimamizi uliofanyika jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa NIT, Profesa Ulingeta Mbamba, alieleza kuwa mkutano huo umeandaliwa kuwakutanisha wataalam wa sekta ya uchukuzi kujadili mbinu bora za kuboresha usafirishaji nchini. "Tafiti na ubunifu ni mihimili mikubwa ya maendeleo ya usafiri nchini. Kongamano hili ni fursa ya kujadili njia za kuboresha sekta hii muhimu kwa uchumi wetu," alisema Profesa Mbamba.

Dk. Prosper Mgaya, Mkuu wa Chuo cha NIT, alisema kuwa kongamano hilo la siku tatu litajadili masuala muhimu ya uchukuzi, ikiwemo usafiri wa anga, majini, na barabara. Aidha, alifafanua kuwa chuo hicho kipo kwenye hatua za mwisho za kupokea cheti kitakachowawezesha kutoa mafunzo ya marubani wenye viwango vya kimataifa. "Tunataka kuhakikisha tunatoa marubani wenye uwezo wa kurusha ndege katika viwango vya kimataifa, na tumejipanga kufanya hivyo kwa ushirikiano na wadau mbalimbali," alieleza Dk. Mgaya.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), Salim Msangi, alithibitisha kuwa serikali imepanga kutumia ndege mbili mpya kwa ajili ya mafunzo ya marubani hao. "Hatua hii itasaidia si tu kupunguza uhaba wa marubani nchini, bali pia kuongeza ushindani wa marubani wetu kwenye soko la kimataifa," alisema Msangi.

Katika upande wa usafiri wa majini, Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbalawa, alibainisha kuwa serikali imewekeza katika Bandari ya Kigoma kwa ujenzi wa meli kubwa ya mizigo yenye uwezo wa kubeba hadi tani 3,000. Mradi huo utaongeza uwezo wa Tanzania kusafirisha bidhaa kwenda nchi jirani, hasa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), na kuimarisha biashara za kikanda.

Hatua hizi zote zinaonesha dhamira ya Tanzania katika kukuza uchumi kupitia sekta ya uchukuzi, ambapo usafiri wa anga na majini utachukua nafasi muhimu katika kufanikisha malengo ya serikali ya muda mrefu ya kuwa kitovu cha usafiri na usafirishaji barani Afrika.