Tume ya Mipango yazungumzia Kongamano la Maandalizi ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050
Na Mwandishi wetu
Dar es Salaam, Tanzania, Juni 4, 2024 – Jina langu naitwa Lawrence Mafuru, ni Katibu Mtendaji Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango, tumewaita hapa waandishi wa habari na wana habari kuzungumza nanyi kuhusu Kongamano la Maandalizi ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050. Kongamano hili litafanyika Jumamosi ya tarehe 8 mwezi wa 6 ,2024 katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kwenye ukumbi wa Nkurumah kuanzia saa tatu kamili asubuhi. Mgeni Rasmi katika Kongamano hilo atakuwa Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kwa kutambua mchango mkubwa mlionao wana habari, waandishi pamoja na vyombo vya habari, tumeona ni vema kuwashirikisha nyie kama wadau muhimu katika kukuza uelewa na kuongeza uhamasishaji wa Kongamano letu la Maandalizi ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050. Ndugu wana habari, tunalo jukumu kubwa la kutoa elimu juu ya Tanzania tuitakayo 2050, ili kuwaandaa vyema wananchi wote kutoa maoni yao ambayo yanachangia kwa asilimia mia moja katika kuiandaa Dira 2050. Kwa maneno na lugha rahisi zaidi, Dira ya Taifa ya Maendeleo ni picha/maono kuhusu mustakabali tarajiwa wa maendeleo ya nchi katika siku za usoni. Dira ya Taifa inapaswa kutupa picha ya matarajio ya nchi kufikia uchumi wa Juu wa Kati (High Middle Income Country) ifikapo mwaka 2050.
Hivyo basi, Tume ya Mipango inasisitiza uelewa na hamasa kwa umma ili kila mtu ashiriki katika kutoa maoni yake. Tunatamani wananchi wote washiriki katika zoezi hili ili tuweze kujibu maswali yafuatayo;-
Je, Dira 2050 inamtaka Mtanzania wa aina gani?
Je, tunataka jamii ya aina gani ya Kitanzania ifikapo 2050?
Je, tunataka nchi ya aina gani ifikapo 2050?
Tume ya Mipango inawahimiza wananchi wote kutoa maoni yao na kuchangia katika mjadala mzima kuhusu Dira 2050. Ushiriki unaweza kuwa katika namna nyingi, ikiwa ni pamoja na kutumia ujumbe mfupi wa simu, majukwaa ya umma, tafiti, mijadala ya mitandao ya kijamii, na mikutano ya kijamii. Maoni ya kila Mtanzania ni ya thamani katika kuandaa Dira 2050 itakayokidhi matarajio na mahitaji yaTaifa.
Jukumu la Waandishi wa Habari na Vyombo vya Habari: Vyombo vya habari vina jukumu muhimu katika kusambaza taarifa, kuwaelimisha wananchi, na kuwezesha mazungumzo. Tunawaomba waandishi wa habari mambo muhimu yafuatayo:
Kuripoti juu ya Hatua zote za Maandilizi ya Dira 2050:
Kuandaa Programu za Elimu: Programu maalum, mahojiano yanayoendeshwa na Tume ya Mipango na Timu Kuu ya Uandishi wa Dira 2050, wataalamu, na mijadala juu ya Dira 2050 zinaweza kuongeza uelewa na ushiriki wa umma.
Kutoa Majukwaa kwa Ushiriki wa Umma: Vyombo vya habari vinapaswa kuruhusu na kuunda njia kwa wananchi kueleza maoni yao, katika vyombo vyenu waweza kuuliza maswali, na kutoa maoni juu ya Dira 2050.
Tume ya Mipango itafanya kazi kwa karibu na waandishi wa habari, wadau wa Maendeleo na wananchi mmoja mmoja ili kuhakikisha kila Mtanzania anafahamishwa, anashiriki, na anachangia kikamilifu katika kuunda mustakabali wa Taifa letu.
Nawashukuru sana kwa usikivu wenu na asanteni kwa kuwa wadau muhimu sana wa uhamasishaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050. Natumai kuwaona tena jumamosi hii kwenye kongamano ambapo tutajadili mengi kwa kina tukiwa na lengo la kuifikia Tanzania Tuitakayo 2050!