Breaking News

Viongozi Watakiwa Kuhubiri Amani na Kuepuka Kauli za Uchochezi

 

Na Mwandishi Wetu

Kijana wa Kitanzania, Dkt David Msuya, ametoa wito kwa viongozi wa kisiasa nchini kutumia lugha za busara wanapozungumza na wananchi ili kulinda amani na mshikamano wa Taifa.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Mei 22,2026 Dkt Msuya amesema licha ya siasa nchini kwenda vizuri, bado zipo changamoto zinazotokana na baadhi ya viongozi kutumia kauli zinazoweza kuleta migawanyiko na maumivu kwa wananchi.

Amesema Watanzania wanahitaji kuona viongozi wakijikita zaidi katika kuzungumzia maendeleo, utekelezaji wa miradi na ustawi wa wananchi badala ya mijadala inayoweza kuchochea chuki na vurugu.

Aidha, amesisitiza kuwa amani ni msingi muhimu wa maendeleo na uwekezaji, akieleza kuwa hakuna wawekezaji watakaokuja katika nchi yenye migogoro na maneno ya uchochezi.

Dkt Msuya pia amewataka viongozi wa dini kuendelea kuiombea Tanzania na kuwashauri viongozi wa kisiasa kuzungumza kwa hekima wanapokutana na wananchi.

Ameongeza kuwa serikali inapaswa kuendelea kusikiliza kero za wananchi na kuchukua hatua kwa wakati ili kuimarisha maendeleo na kuondoa malalamiko yasiyo ya lazima.

“Watanzania wote ni ndugu, tunapaswa kuhubiri upendo, mshikamano na amani kwa ajili ya ustawi wa Taifa letu,” amesema Dkt Msuya.