SOKO LA HISA LA DAR ES SALAAM MWENYEJI WA KONGAWANO LA SUKUK YA SERIKALI YA UGANDA.
Na Mwandishi Wetu
Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) lina furaha kuwa mwenyeji wa Kongamano la Sukuk ya Serikali ya Uganda (Uganda Sovereign Sukuk Roadshow) kwa ushirikiano na Wizara ya Fedha, Mipango na Maendeleo ya Uchumi ya Uganda pamoja na kampuni ya Yusra Sukuk Company Limited.
Kongamano hili litawapa wawekezaji na wadau wa masoko ya mitaji fursa ya kujifunza zaidi kuhusu Sukuk ya Miundombinu ya Serikali ya Uganda yenye thamani ya Euro Milioni 205, ikiwa na chaguo la ziada (Green Shoe Option) la Euro Milioni 30, kama sehemu ya mpango mpana wa utoaji wa Sukuk wenye thamani ya Euro Milioni 495.
Mambo muhimu kuhusu Sukuk hii ni pamoja na:
Sukuk ya Serikali inayoweza kuuzwa na kununuliwa na inayolindwa na rasilimali (Asset-backed)
Faida (coupons) na kiasi cha ukombozi vimewekewa bima ya Takaful
Mchakato wa ukadiriaji wa mikopo na Wakala wa Kimataifa wa Ukadiriaji wa Kiislamu (IIRA) unaendelea
Msamaha wa kodi kwenye malipo ya faida kwa wawekezaji
Kikao hicho kiliongozwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Mipango na Maendeleo ya Uchumi ya Uganda, Bw. Patrick Ocailap, kikikutanisha wadau wa soko la upili, wawekezaji wa taasisi, na wadau wakuu wa sekta ya fedha ili kuchunguza fursa za mitaji ya Kiislamu kikanda.
