PUMA ENERGY TANZANIA KUZINDUA PROGRAMU YA PRIS
Na Mwandishi wetu -Dar es Salaam
Mkurugenzi Mkuu wa Puma Energy Tanzania, Bi. Fatma Abdallah amesema kampuni hiyo inaunga mkono Mfumo wa Kimkakati wa Uchumi wa Dijitali Tanzania (2024–2034), unaolenga kuiweka nchi kama kitovu cha kidijitali cha kikanda kupitia uimarishaji wa miundombinu, kupanua ujumuishaji wa kifedha pamoja na kuchochea ukuaji wa uchumi.
Bi. Abdallah amesema hayo leo jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu uzinduzi wa Programu ya PRIS App ya Puma Energy unaotarajiwa kufanyika kesho.
Programu hiyo inalenga kuwazawadia wateja wanaofanya manunuzi ya mafuta, vilainishi pamoja na bidhaa mbalimbali zinazopatikana katika maduka ya kampuni hiyo yaliyopo kwenye vituo vyake nchini kote.
Aidha, amesema Puma Energy inaendesha zaidi ya vituo 2,201 vya rejareja na kuhudumia viwanja vya ndege 107 duniani, huku lengo kuu likiwa ni kuhamasisha jamii ili kuendeleza ukuaji na mafanikio ya kiuchumi. Ameeleza kuwa kampuni hiyo inalenga kuongeza mara dufu shughuli zake ifikapo mwaka 2030 kwa dhamira ya kuchangia zaidi ukuaji wa uchumi wa nchi.
“Kwa miaka mitatu iliyopita pekee, Puma Energy Tanzania imechangia zaidi ya shilingi trilioni 1.4 kwa Serikali kupitia kodi na ushuru. Mwaka 2025 kampuni ilitangaza gawio la shilingi bilioni 21, hatua iliyoimarisha mapato ya kifedha yanayotokana na umiliki wa Serikali wa asilimia 50 kupitia Msajili wa Hazina,” amesema Bi. Abdallah.
Ameongeza kuwa baada ya uzinduzi wa mafanikio wa mfumo huo katika nchi za Zimbabwe mwezi Novemba 2025, Malawi mwezi Februari 2026 na Botswana mwezi Machi 2026, Tanzania sasa inakuwa soko la nne barani Afrika kutumia mfumo huo wa kidijitali.
Mkurugenzi huyo pia amebainisha kuwa kampuni hiyo inatoa huduma ya mafuta ya ndege katika viwanja nane vya ndege nchini, ikiwemo viwanja vitatu vya kimataifa na vitano vya kitaifa, huku akisisitiza kuwa upatikanaji wa mafuta nchini ni wa kutosha kuhudumia mahitaji ya Watanzania.
Mkutano huo pia ulihudhuriwa na Bw. Sulpis Mmasi, Meneja Mauzo ya Rejareja wa Puma Energy Tanzania pamoja na Bi. Lilian Kanora kutoka Idara ya Masoko ya kampuni


