Kichwa cha Marehemu James Temba chapatikana Kitunda Kibeberu
Na Mwandishi wetu- Dar es salaam
Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam limetoa wito kwa wananchi kuendelea kuwa watulivu na kuviachia vyombo vya dola kutekeleza majukumu yake kitaalamu pindi yanapotokea matukio ya kihalifu, huku likionya dhidi ya tabia ya kusambaza taarifa za upotoshaji zinazoweza kuchelewesha upelelezi na kuzua taharuki kwa jamii.
Wito huo umetolewa leo Mei 13, 2026 wakati Jeshi hilo likitoa taarifa ya maendeleo ya uchunguzi wa mauaji ya James Rogers Temba, mwanafunzi wa mwaka wa pili wa Chuo cha Institute of Finance Management (IFM), aliyefariki katika mazingira ya kutatanisha.
Kwa mujibu wa Polisi, baada ya uchunguzi wa kina kufanyika, sehemu ya kichwa cha marehemu iliyokuwa imepotea imepatikana katika eneo la Kitunda Kibeberu, Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam, ikiwa imefukiwa ardhini na watu wanaodaiwa kutekeleza uhalifu huo.
Jeshi hilo limeeleza kuwa jumla ya watuhumiwa watano wanashikiliwa kuhusiana na tukio hilo, akiwemo Said Ally maarufu kama “Side”, mwenye umri wa miaka 31, anayefahamika kuwa mganga wa kienyeji na mkazi wa Kitunda Kibeberu.
“Jeshi la Polisi linaendelea kulaani tukio hili baya na la kusikitisha, huku likiendelea kufuatilia kwa karibu shauri hili pamoja na mengine yanayohusiana na uhalifu,” amesema SACP MULIRO
Aidha, Muliro amewashukuru wananchi pamoja na mamlaka mbalimbali za uchunguzi wa kisayansi kwa ushirikiano na utoaji wa taarifa zilizosaidia kufanikisha hatua za uchunguzi zinazoendelea.
Polisi imesema taratibu za kisheria zinaendelea kukamilishwa ili mamlaka husika ziweze kuchukua hatua zaidi dhidi ya watuhumiwa waliokamatwa.
