Breaking News

Diwani Mboga Apongeza Vijana Makangarawe kwa Kuimarisha Umoja Kupitia Michezo

 

Na Hawa Ismail-Dar es Salaam

Diwani wa Kata ya Makangarawe, Fadhili Mboga, amewapongeza vijana wa kata hiyo kwa kujitokeza kwa wingi kushiriki mashindano ya mpira wa miguu ya “Diwani Mboga Chandimu Cup”, akisema mashindano hayo yamekuwa chachu ya kuimarisha umoja, mshikamano na kuibua vipaji vya michezo kwa vijana.

Mboga amesema hayo leo Mei 24, 2026 jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya kukabidhi zawadi kwa timu zilizofika fainali, ambapo timu ya Stanford iliibuka bingwa baada ya kuifunga timu ya Bondeni kwa mikwaju ya penalti. Katika mashindano hayo, diwani huyo alikabidhi mbuzi watatu kwa timu ya Stanford kama zawadi ya ushindi pamoja na timu ya Bondeni mbuzi wawili kwa kuwa mshindi wa pili.

Amesema kupitia mashindano hayo wamefanikiwa kutambua vijana wenye vipaji vikubwa vya mpira wa miguu, wakiwemo washambuliaji na makipa wenye uwezo mkubwa ambao wanaweza kukuza vipaji vyao na kufikia hatua za juu zaidi kimichezo.

“Tumefanikiwa kuibua vipaji vya vijana wetu kupitia mashindano haya ya ‘Diwani Mboga Chandimu Cup’, na tumeona vijana wengi wenye uwezo mkubwa wa kucheza mpira wa miguu pamoja na makipa wazuri sana kutoka katika kata yetu ya Makangarawe,” amesema Mboga.

Aidha, imeelezwa kuwa Diwani Mboga amekuwa mstari wa mbele katika kuwaunga mkono vijana wa Makangarawe kupitia michezo pamoja na kutoa hamasa kwa wanafunzi wa Shule za Msingi Yombo Dovya na Jitihada kushiriki michezo ili kukuza vipaji na kujenga afya bora.

Fainali ya mashindano hayo ilifanyika katika Uwanja wa Makaburi ya City, Makangarawe, ambapo wananchi na vijana mbalimbali walijitokeza kushuhudia michezo hiyo iliyotajwa kuwa sehemu muhimu ya kuhamasisha jamii kupenda na kuthamini michezo.

Katika hatua nyingine, Mwenyekiti wa TEFA, Ally Kamtande, alikabidhi mpira mmoja kwa kila timu iliyoshiriki mashindano hayo huku akisisitiza umuhimu wa kuendelea kuwaunga mkono vijana katika sekta ya michezo.

Kamtande pia alimpongeza Diwani Mboga kwa juhudi zake za kuendeleza michezo Makangarawe, akieleza kuwa uwepo wa wahudumu wa huduma ya kwanza katika mashindano hayo umeonesha namna viongozi wanavyothamini afya na usalama wa wachezaji wakati wa michezo.