Viongozi Msiikimbie Miradi Dhaifu Katika Maandalizi ya Mapokezi ya Mwenge wa Uhuru
Na Mwandishi wetu -MARA
“Unapobaini mradi A katika wilaya yako una changamoto, unazitatua vizuri na kwa uhakika na siyo kuweka cosmetic surgery au kuukimbia, nataka Mkoa wa Mara tuitambue miradi yetu vizuri, tuyabaini madhaifu na tuyafanyie kazi wakati na kwa uhakika na hili ndilo jukumu letu ili Mwenge wa Uhuru ukija na kama unakuta tulipofikia na tena kama bado kuna madhaifu Mwenge wa Uhuru unayachoma yale madhaifu.”
Haya ni maelekezo ya Mkuu wa Mkoa wa Mara mheshimiwa Kanali Evans Alfred Mtambi Aprili 30, 2026 Musoma Mjini katika kikao cha Mkoa wa Mara cha maandalizi ya Mapokezi ya Mwenge wa Uhuru.
Akiendelea kutoa msisitizo kikaoni humo Kanali Mtambi alisema:
“Viongozi wezangu najua kumekuwa na utaratibu wa kuikimbia miradi yenye udhaifu na kuiweka miradi yenye hali nzuri na huku baadhi ya miradi maeneo mengine kuikimbia kisha kuichagua miradi mipya ambayo tunaona haina madhaifu, hiyo yote ni miradi ya wananchi lazima madhaifu yatambulike na yatatuliwe mara moja kila mradi uwe vizuri.”
Kanali Mtambi alitoa nafasi ya kila Wilaya kutoa taarifa ya maandalizi ya mapokezo ya Mwenge wa Uhuru huku kila wilaya ilidokeza kuwa maandalizi yanaendelea yakiwa kwa kiwango cha juu.
Mheshimiwa Kanali Mtambi akiongoza kikao hiki pia aliwapongeza wakuu wa Wilaya za Mkoa wa Mara kwa kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa weledi huku wakishirikiana na Wakurugenzi na wakuu wote wa taasisi za umma pamoja na wafanyakazi na wananchi wa mkoa huu.
Mandhari ya hiki kikao yalionesha kilihudhuriwa na viongozi kadhaa kutoka Vyombo vya Ulinzi na Usalama Mkoa wa Mara na huku Katibu wa Kikao akiwa Katibu Tawala Mkoa wa Mara Ndugu Gerald Musabila Kusaya ambaye ndiyo aliyekuwa akisoma ajenda moja baada ya nyingine tangu mwanzo wa kikao hadi tamati.
Awali akitoa taarifa ya tarehe za uwepo wa Mwenge wa Uhuru kwa Mkoa wa Mara Mratibu wa Mwenge wa Uhuru kwa Mkoa wa Mara mwaka wa 2026 Ndugu Fidel Balagaye alisema:
“Mwenge wa Uhuru unatarajiwa kukimbizwa Mkoani Mara kwa siku kenda tangu Agosti Mosi 2026 na kukabidhiwa kwa Mkoa wa Mwanza Agosti 10 ya 2026.”
Wakati haya yakiendelea hapa Musoma hali ya hewa ya mji wa Musoma ni nyuzi joto 27, unyevunyevu ni asilimia sufuri, ujirani na mvua ni wa asilimia 63 na upepo ukivuma kwa KM 8 kwa saa.
“Viongozi Msiikimbie Miradi Dhaifu Katika Maandalizi ya Mapokezi ya Mwenge wa Uhuru.”




