Breaking News

TTCL YATENGENEZA FAIDA YA BILIONI 22, KUTOKA KWENYE HASARA YA BILIONI 24 — WAZIRI KAIRUKI

 

Na Mwandishi- Dodoma 

Serikali imesema mageuzi yanayoendelea katika Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) yameanza kuleta matokeo chanya, baada ya shirika hilo kutengeneza faida kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni.  

Akiwasilisha hitimisho la hoja ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari bungeni jijini Dodoma, Waziri Angellah Kairuki amesema TTCL sasa imetengeneza faida ya shilingi bilioni 22, ikilinganishwa na hasara ya takribani shilingi bilioni 24 iliyorekodiwa miaka ya nyuma.  

Kwa mujibu wa taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka 2024/2025, mabadiliko hayo yamechangiwa na hatua za Serikali kuimarisha uwezo wa taasisi zake za mawasiliano kupitia uwezeshaji wa kifedha na maboresho ya kiutendaji.  

Waziri Kairuki amssema kwa mwaka wa fedha 2025/2026, Serikali imezipatia TTCL, Shirika la Posta na Tume ya Taifa ya TEHAMA jumla ya shilingi bilioni 31.5, fedha ambazo zimeziwezesha taasisi hizo kuimarika katika utekelezaji wa majukumu yao.  


Amesema mafanikio ya TTCL ni ishara ya mwelekeo mpya wa shirika hilo, na kwamba Serikali inaamini hatua hiyo itaongeza uwezo wa TTCL kuchangia mapato ya taifa kupitia gawio.  

Aidha, Waziri Kairuki amebainisha kuwa Serikali imeshaandaa mkakati wa miaka 10 wa kulifanya TTCL kujiendesha kibiashara kwa ufanisi zaidi, hatua inayolenga kuongeza mapato, kupanua huduma na kulifanya shirika hilo kuwa miongoni mwa watoa huduma bora katika soko la mawasiliano.