MHE. MIZENGO PINDA, AWAFUNDA WATAALAMU WA JESHI LA MAGEREZA KUPITIA MAFUNZO YA UFUGAJI NYUKI DODOMA
Na. Ssgt Mawazo Mtondo - Dodoma.
Zaidi ya wataalamu 30 wa ufugaji nyuki kutoka Jeshi la Magereza, waliotoka mikoa mbalimbali nchini, wametembelea na kupata mafunzo ya vitendo katika shamba darasa la Waziri Mkuu Mstaafu, Mhe. Mizengo Pinda, lililopo Zuzu, jijini Dodoma.
Akizungumza na wataalamu hao, Mhe. Pinda alisema ameridhishwa na hatua zinazochukuliwa na Jeshi la Magereza katika kuboresha mifumo ya urekebishaji wa wafungwa kupitia miradi ya uzalishaji, ikiwemo ufugaji nyuki. Alibainisha kuwa ni jambo la faraja kuona taasisi hiyo inaweka mikakati madhubuti ya kuwaandaa wafungwa kurejea katika jamii wakiwa na ujuzi wa kujitegemea.
Aliongeza kuwa, pamoja na hatua ya Serikali kusamehe baadhi ya wafungwa, ni muhimu kuhakikisha kuwa wanaachiwa wakiwa na maandalizi ya maisha ya baada ya kifungo. Alisema jitihada za kuwawezesha mitaji midogo kupitia mikopo ni hatua sahihi itakayowasaidia kuanzisha shughuli za kiuchumi na kujikwamua kimaisha.
Aidha, Mhe. Pinda alieleza kuwa Tanzania imebarikiwa kuwa na rasilimali nyingi za misitu na mazingira rafiki kwa ufugaji nyuki, akitaja uwepo wa makundi makubwa ya nyuki yanayofikia zaidi ya milioni 10. Alisisitiza umuhimu wa kuendeleza sekta hiyo kwa kuwa nyuki wana mchango mkubwa katika uchavushaji wa mimea na uhifadhi wa mazingira.
Alipendekeza kuandaliwa kwa kongamano litakalowakutanisha wadau wa ufugaji nyuki pamoja na wataalamu kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), ili kuongeza uelewa na kubadilishana uzoefu utakaosaidia kuboresha sekta hiyo ndani ya Jeshi la Magereza.
Kwa upande wake, Kamishna wa Huduma za Urekebishaji wa Jeshi la Magereza, CP Amina Kavirondo, alisema kuwa Jeshi hilo limefanya mapitio ya kina ya mifumo yake ya urekebishaji na kuandaa mwongozo mpya unaolenga kuboresha huduma hizo kwa kuanzia hatua ya kwanza mfungwa anapoingia gerezani.
Alifafanua kuwa mchakato wa urekebishaji unahusisha hatua kuu nne ambazo ni mapokezi ya mfungwa (ikiwemo utambuzi, uainisho na utenganisho), utekelezaji wa kifungo, maandalizi ya kumaliza kifungo, na hatimaye utangamanisho katika jamii.
“Tunafanya uchambuzi wa kina kwa kila mfungwa ili kubaini mahitaji yake ya urekebishaji, hatua inayotuwezesha kumpangia programu sahihi kulingana na hali yake,” alisema CP. Kavirondo, akifananisha mchakato huo na huduma za afya ambapo mgonjwa hupimwa kwanza kabla ya kupewa tiba stahiki.
Aliongeza kuwa mafunzo ya ufugaji nyuki ni sehemu ya jitihada za kuwajengea uwezo wataalam wa Jeshi la Magereza ili waweze kuwafundisha wafungwa stadi zitakazowawezesha kujitegemea wanapomaliza vifungo vyao.
Aidha, alibainisha kuwa Jeshi la Magereza linaendelea kushirikiana na taasisi mbalimbali ikiwemo Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) na Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA) katika kutambua na kuendeleza ujuzi wa wafungwa kupitia mafunzo ya vitendo na nadharia.
Alisema kupitia ushirikiano huo, wafungwa wanaopata mafunzo huwezeshwa kupata vyeti vinavyotambulika, hatua inayowaongezea fursa za ajira na kujiajiri pindi wanapomaliza vifungo vyao.
CP Kavirondo alisisitiza kuwa lengo kuu la maboresho hayo ni kuhakikisha Jeshi la Magereza linapimwa kwa mafanikio ya kupunguza idadi ya wafungwa wanaorudia makosa, kwa kuwajengea uwezo askari na wataalamu wanaosimamia programu za urekebishaji.
Aliongeza kuwa kwa sasa Jeshi linaendelea na mafunzo ya kuwajengea uwezo askari juu ya mitaala mipya ya programu za urekebishaji, ili kuongeza ufanisi katika kuwasaidia wafungwa kupata ujuzi utakaowawezesha kujitegemea na kujiunganisha kikamilifu na jamii baada ya kutumaliza vifungo vyao.








