DC UBUNGO AWATAKA VIJANA KUZINGATIA UZALENDO NA KUPINGA RUSHWA
Na Mwandishi Wetu – Dar es Salaam
Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Mheshimiwa Albert Msando, amewakumbusha vijana nchini kuzingatia uzalendo, kuwa na ukakamavu pamoja na kujitolea kulinda Taifa lao, huku akiwataka kuepuka kujihusisha na vitendo vya rushwa.
Mheshimiwa Msando ametoa kauli hiyo leo katika semina iliyofanyika katika Manispaa ya Ubungo, jijini Dar es Salaam, sambamba na uzinduzi wa jukwaa la Vijana (Vijana Platform).
Aidha, amesema kuwa pamoja na majukumu mengine, Serikali ina jukumu la kuwaandaa vijana kuwa na ajira endelevu kupitia sekta mbalimbali. Ameeleza kuwa Serikali pia inaendelea kuboresha huduma za afya, hususan huduma ya mama na mtoto kwa kuhakikisha upatikanaji wa dawa na vifaa tiba vya kutosha.
Katika sekta ya elimu, Mheshimiwa Msando amesema Serikali inalenga kuongeza fursa za elimu kwa vijana kwa kujenga shule katika kila kata, hatua itakayochangia kuongeza idadi ya vijana wanaopata elimu kwa kiwango kikubwa zaidi.
Vilevile, amebainisha kuwa Serikali imeendelea kuongeza upatikanaji wa mikopo kwa vijana pamoja na nafasi za ajira, ambapo hadi sasa zaidi ya vijana laki tisa hadi milioni moja na laki moja wamepata ajira Serikalini, mafanikio yanayotokana na utekelezaji wa sera ya ajira nchini.
