Watanzania 236 Waliokwama Dubai Warejeshwa Nyumbani, Wasimulia Hali ya Taharuki Mashariki ya Kati
Watanzania 236 waliokuwa wamekwama katika miji ya Dubai na Abu Dhabi wamewasili salama nchini baada ya kurejeshwa kwa ndege maalumu iliyoratibiwa na Serikali ya Tanzania kufuatia mvutano wa kijeshi unaoendelea katika ukanda wa Mashariki ya Kati.
Mvutano huo unaohusisha mataifa ya Israel, Marekani na Iran umeendelea kuzua taharuki katika eneo hilo na kuathiri maisha ya watu wengi, wakiwemo raia wa mataifa mbalimbali wanaoishi au kufanya kazi katika nchi za Ghuba.
Furaha na hisia kali zilitawala katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam, ndugu na jamaa walipokusanyika kuwapokea wapendwa wao waliorejea nyumbani baada ya siku kadhaa za wasiwasi kuhusu usalama wao.
Baadhi ya waliokuwa wakisubiri kuwapokea ndugu zao hawakuweza kuficha hisia zao walipowaona wakitoka katika jengo la abiria wakiwa salama. Mama mmoja aliyempokea mwanawe aliyekuwa amekwama Dubai alisema amekuwa akiomba kila siku ili Mungu amlinde mtoto wake.
“Nimekuwa nikisali kila siku nikimuomba Mungu amlinde mwanangu. Leo nimemwona tena akiwa salama, ni jambo la kumshukuru sana Mungu,” amesema.
Baadhi ya Watanzania waliorejea wamesema waliishi kwa tahadhari kubwa kutokana na hali ya hofu iliyotanda kufuatia taarifa za mashambulizi na mvutano wa kijeshi katika ukanda huo.
John Bina, mmoja wa waliorejea, amesema katika kipindi hicho wakazi wengi walikuwa wakifuatilia kwa karibu taarifa za usalama huku baadhi yao wakiepuka kutoka nje bila sababu za msingi.
“Hali ilikuwa ya wasiwasi sana kwa sababu kulikuwa na taarifa za mashambulizi katika maeneo mbalimbali ya ukanda huo. Watu wengi walikuwa wakifuatilia habari kila muda ili kujua kinachoendelea,” amesema Bina.
Kwa upande wake, Princes Mwakatobe amesema taharuki ilionekana zaidi miongoni mwa wageni wanaoishi katika miji hiyo, huku shughuli za kijamii zikianza kupungua na mikusanyiko mikubwa kuepukwa kutokana na tahadhari za kiusalama.
“Tulikuwa tunaishi kwa tahadhari kubwa sana. Hata kutoka nje au kusafiri ilikuwa ngumu kwa sababu ya hofu iliyokuwapo,” amesema Mwakatobe.
Waliorejea walisema walipata faraja kubwa baada ya kupata taarifa kuwa Serikali ya Tanzania imeandaa ndege maalumu kwa ajili ya kuwarejesha nyumbani, kwani wengi wao walikuwa wameanza kuwa na hofu ya kuendelea kukaa katika eneo hilo bila uhakika wa usalama.
Akizungumzia operesheni hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa Uendeshaji wa Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL), Arif Jinnah, amesema mpango wa kuwarejesha Watanzania hao ulitekelezwa kwa ushirikiano wa karibu kati ya Serikali na mamlaka za anga za nchi husika.
Amesema mara baada ya kupata taarifa kuhusu uwepo wa Watanzania waliokuwa katika mazingira hatarishi, serikali ilichukua hatua za haraka kuratibu safari maalumu ya ndege ili kuhakikisha wanarejeshwa nyumbani kwa usalama.
“Lengo lilikuwa kuhakikisha raia wetu wanarudi nchini salama. Serikali imeonyesha dhamira ya kuwalinda Watanzania popote walipo,” amesema Jinnah.
Ameongeza kuwa operesheni hiyo ilifanyika kwa tahadhari kubwa ili kuhakikisha safari inafanyika kwa usalama licha ya changamoto za kiusalama zilizokuwa zikijitokeza katika ukanda wa Mashariki ya Kati.





