SACP. MBEZI AWAONGOZA MAAFISA, ASKARI NA WATUMISHI WASIO ASKARI WANAWAKE KUTOA MSAADA KWA WAZEE NA WATOTO WENYE MAHITAJI MAALUM
Ssgt Mawazo Mtondo na CPL Rose Marwa - Dodoma.
Katika kuelekea maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, leo Machi 7, 2026, Msemaji wa Jeshi la Magereza, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Magereza (SACP) Elizabeth Mbezi, amewaongoza Maafisa, Askari na watumishi wasio Askari wanawake wa Jeshi hilo kutoka Makao Makuu pamoja na wengine kutoka Magereza mbalimbali yaliyopo Mkoa wa Dodoma kutoa msaada wa mahitaji muhimu kwa wazee na watoto wenye uhitaji waliopo katika kituo cha Masista wa Missionari wa Huruma wa Teresa – Nyumba ya Furaha na Upendo, kilichopo Hombolo, Jijini Dodoma.
Akizungumza wakati wa kukabidhi msaada huo, Mkuu wa msafara huo na Msemaji wa Jeshi la Magereza, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Magereza (SACP) Elizabeth Mbezi, alisema kuwa askari wanawake wamejitoa kwa hali na mali katika kufanikisha malengo ya kusaidia makundi yenye uhitaji katika jamii.
Aliongeza kuwa jitihada hizi zinaonesha dhamira ya askari wanawake kushiriki kikamilifu katika shughuli za kijamii, sambamba na kuunga mkono maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani.
Kwa upande wake, msimamizi wa kituo hicho Bwana Joseph Tarimo alitoa shukrani kwa watumishi wa Jeshi la Magereza kwa msaada huo, akisema kuwa umeleta faraja kubwa kwa wazee, watoto wenye uhitaji ambao wanakaanao katika kituo hicho. Alieleza kuwa kitendo hicho kinaonesha wazi kwamba vyombo vya ulinzi na usalama vinaendelea kuwa karibu na jamii ya watu wenye uhitaji.
Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani hufanyika kila mwaka tarehe 8 Machi. Kwa mwaka huu, maadhimisho hayo yanatarajiwa kufanyika katika Wilaya ya Kongwa, yakilenga kutambua mchango wa wanawake katika maendeleo ya jamii pamoja na kuhamasisha usawa wa kijinsia duniani.


