Breaking News

RC CHALAMILA ATOA ONYO LA MOTO KWA WANAOKWEPA MALEZI: “HAITAVUMILIWA!” ‎

 

Albert Chalamila Mkuu wa Mkoa Dar es Salaam 


Na Mwandishi Wetu- Dar es Salaam 

‎Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, amewataka wazazi na walezi ambao wenza wao wakwepa majukumu ya malezi kujitokeza ofisini kwake kushughulikia migogoro yao, akisisitiza kuwa serikali haitavumilia uzembe unaoathiri ustawi wa watoto.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Machi 2,2026  Chalamila amesema kumekuwepo na ongezeko la malalamiko kuhusu migogoro ya ndoa na malezi, ambapo baadhi ya wazazi wamekuwa wakikwepa wajibu wa kuwalea na kuwahudumia watoto wao.

‎Ameeleza kuwa ofisi yake imepokea kesi kadhaa zinazohusu matunzo ya watoto, migogoro ya kifamilia na kutotekelezwa kwa makubaliano ya kisheria, hali inayosababisha madhara kwa watoto na familia kwa ujumla.

‎Chalamila amesisitiza kuwa serikali ya mkoa itaendelea kusimamia haki za watoto na kuhakikisha kila mzazi anatimiza wajibu wake kwa mujibu wa sheria. Alionya kuwa hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya wale watakaobainika kukaidi maelekezo au kukiuka sheria.

‎Aidha, amewahimiza wananchi kutafuta suluhu ya migogoro yao kwa njia ya mazungumzo na kufuata taratibu za kisheria ili kulinda maslahi ya watoto na kudumisha amani katika familia.

‎Hata hivyo ameongeza kuwa ofisi yake iko tayari kusikiliza na kusaidia wananchi wanaokabiliwa na changamoto za kifamilia ili kuhakikisha ustawi wa jamii unaimarika.