mradi wa uhifadhi wa matumbawe waanzishwa, wadau wahimizwa kulinda rasilimali za bahari
Na Mwandishi Wetu- Dar es Salaam
Meneja wa mradi na msimamizi wa matumbawe, Godfrey Mbutura, amesisitiza umuhimu wa kutunza matumbawe, mikoko pamoja na nyasi za bahari akibainisha kuwa rasilimali hizo ndizo zinazoleta uhai wa bahari.
Amesema hayo leo Machi 24, 2026 jijini Dar es Salaam wakati wa kikao kazi na wadau wa uhifadhi wa mikoko, ambapo alieleza kuwa Tanzania imekuwa kinara katika uhifadhi wa matumbawe na ina uwezo mkubwa wa kustahimili athari za mabadiliko ya tabianchi.
“Matumbawe yana faida kubwa kwa jamii, ambapo zaidi ya asilimia 70 ya watu wanaoishi ukanda wa pwani wanategemea huduma zake. Hata hivyo, changamoto kubwa ni uvuvi haramu unaofanywa kwa mabomu na nyavu zisizoruhusiwa, hali inayosababisha uharibifu mkubwa wa matumbawe,” amesema Mbutura.
Aidha, amesema mradi huo utasaidia kuwaunganisha wadau mbalimbali na kutoa elimu ya uhifadhi, akisisitiza kuwa matumbawe huchukua zaidi ya miaka 100 kukua na kuwa miamba imara, hivyo yanahitaji kulindwa kwa uangalifu mkubwa.
Kwa upande wake, mshiriki kutoka Zanzibar, Bahati Issa Suleiman, amesema ushiriki wake katika mradi huo unalenga kupata mrejesho wa kitaalamu kwa ajili ya kuimarisha uhifadhi wa matumbawe pamoja na kuwashirikisha wavuvi wadogo katika juhudi hizo. Ameongeza kuwa elimu inayotolewa kupitia mradi huo tayari imeanza kuleta matokeo chanya, huku hali ya bahari ikiendelea kuimarika.
Naye Afisa Uvuvi wa Mkoa wa Tanga, Issa Khatibu, amesema mradi huo utasaidia kupunguza changamoto za uharibifu wa matumbawe katika mkoa huo, ambao umeathirika kwa kiasi kikubwa, na kuleta suluhisho la kudumu kupitia ushirikishwaji wa jamii na wadau mbalimbali.






