Breaking News

Diwani Makangarawe Ajipanga Kutatua Changamoto za Shule Yombo Dovya na Jitihada, Amshukuru Rais Samia kwa Ujenzi wa Sekondari ya Kisasa ya ghorofa

 

Diwani wa kata ya Makangarawe Fadhili Mboga 

Na Hawa Ismail, Dar es Salaam

Diwani wa Kata ya Makangarawe, Fadhili Mboga, amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa juhudi zake za kuboresha sekta ya elimu katika kata hiyo iliyopo Wilaya ya Temeke, jijini Dar es Salaam.

Mboga ametoa shukrani hizo Machi 13, 2026 wakati wa ziara yake ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa Shule ya Sekondari Makangarawe pamoja na miundombinu katika Shule za Msingi Yombo Dovya na Jitihada. Amesema ameanza kuchukua hatua za kutatua changamoto mbalimbali zinazozikabili shule hizo ikiwemo upungufu wa madawati, uboreshaji wa miundombinu, ujenzi wa sakafu za kisasa pamoja na kuongeza viti na meza kwa walimu.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mboga alisema ujenzi wa Shule ya Sekondari Makangarawe ni hatua muhimu katika kuboresha upatikanaji wa elimu kwa watoto wa kata hiyo.





“Namshukuru sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa juhudi kubwa alizoweka kuhakikisha elimu bora inapatikana kwa kila mwananchi wa Makangarawe. Serikali imetujengea shule ya kisasa ya ghorofa tano yenye jumla ya madarasa 20, na mkandarasi anatarajiwa kukabidhi mradi huo ifikapo mwaka 2028 ili wanafunzi wetu waanze kusoma hapa hapa Makangarawe,” alisema Mboga.

Katika ziara hiyo, Mboga pia alikagua maendeleo ya ujenzi wa Shule ya Sekondari Makangarawe ambapo alibaini kuwa ujenzi unaendelea vizuri na umefikia hatua ya kuridhisha.

Aidha, alitembelea Shule za Msingi Jitihada na Yombo Dovya na kukagua miundombinu mbalimbali ikiwemo madarasa, nyumba za walimu, maktaba ya shule, ofisi za walimu pamoja na vyoo vya wanafunzi na walimu.

Kwa upande wake, Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Makangarawe, Julius Mkada, alimshukuru Rais Samia kwa kutatua changamoto ya ukosefu wa shule ya sekondari katika kata hiyo kupitia ujenzi wa shule ya kisasa ya ghorofa tano yenye madarasa 20.

Alisema kukamilika kwa shule hiyo kutasaidia wanafunzi waliokuwa wakisoma katika Shule za Msingi Yombo Dovya na Jitihada kupata nafasi ya kuendelea na masomo yao karibu na makazi yao badala ya kusafiri umbali mrefu kutafuta shule za sekondari.

Katika hatua nyingine, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Yombo Dovya, Salum Gawaza, alisema shule hiyo yenye zaidi ya miaka 50 ina wanafunzi 1,911 na walimu 38, ambapo watatu ni walimu wa elimu maalumu.

Alifafanua kuwa kutokana na upungufu wa walimu, shule hiyo inasaidiwa na walimu wanane wa kujitolea ambao hulipwa kwa michango ya wazazi ili kusaidia kuendesha shughuli za ufundishaji.

Gawaza alisema shule hiyo inahitaji jumla ya madarasa 43 lakini kwa sasa ina madarasa 24 pekee, matatu kati yake yakiwa ya elimu maalumu, hali inayosababisha darasa moja kuwa na wanafunzi kati ya 80 hadi 100.

Aliongeza kuwa shule hiyo inahitaji matundu 86 ya vyoo kwa wanafunzi lakini yaliyopo ni 38 tu, huku walimu wakiwa na matundu sita pekee — mawili kwa walimu wa kiume na manne kwa walimu wa kike.

“Tunaupungufu wa madarasa 16 na kwa upande wa madawati tunahitaji 637 lakini yaliyopo ni 360 tu, hivyo kuna upungufu wa madawati 277. Hali hii inasababisha baadhi ya wanafunzi kukaa chini wakati wa masomo,” alisema Gawaza.

Wakazi wa Makangarawe wameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa ujenzi wa Shule ya Sekondari Makangarawe wakisema hatua hiyo itasaidia kupunguza changamoto ya wanafunzi kusafiri umbali mrefu kutafuta elimu ya sekondari nje ya kata hiyo.