Breaking News

UONGOZI UBUNGO WATOA HAKIKISHO KULINDA MASLAHI YA WATUMISHI KUPITIA BAJETI YA 2026/2027

 

Na Hawa Ismail- Dar es Salaam 

Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo, Aron Kagurumjuli, amesema uongozi wa halmashauri hiyo umejipanga kikamilifu kuhakikisha maslahi ya watumishi yanalindwa ipasavyo, sambamba na kuwahakikishia watumishi wote wanaostahili kupata huduma zinazotokana na bajeti ya Manispaa wanazipata kwa mujibu wa mipango iliyowekwa.

Kagurumjuli alitoa kauli hiyo wakati wa kikao cha kujadili bajeti ya mwaka wa fedha 2026/2027, akisisitiza kuwa halmashauri imeweka mikakati madhubuti ya usimamizi wa rasilimali ili kuhakikisha haki na stahiki za watumishi zinatekelezwa bila vikwazo.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Walimu Manispaa ya Ubungo, Mwalimu Sostenence Haule, alisema kikao hicho kililenga kupitia bajeti hiyo na kutoa ushauri kuhusu maeneo yanayogusa moja kwa moja maslahi ya watumishi wa umma pamoja na wananchi kwa ujumla.

Alieleza kuwa tathmini ya awali inaonesha bajeti hiyo imezingatia mahitaji ya wananchi na wafanyakazi, huku akibainisha kuwa utekelezaji wake unatarajiwa kufungua fursa mbalimbali za maendeleo katika halmashauri hiyo.

“Ukiangalia bajeti hii, kwa kweli imekidhi mahitaji na matarajio ya wananchi pamoja na wafanyakazi. Imegusa maeneo yote muhimu na itaifungulia Manispaa ya Ubungo milango ya maendeleo yenye tija,” alisema Haule.

Aidha, aliwataka watumishi wa halmashauri hiyo kutokuwa na hofu kuhusu utekelezaji wa bajeti, akieleza kuwa ongezeko la mapato ya ndani limeongeza uwezo wa Manispaa kutekeleza miradi na kulipa stahiki mbalimbali kwa wakati.

Naye Kiongozi wa Wafanyakazi na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji Taifa (TALB) wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa Tanzania, Dkt. Ally Njama, alisema bajeti iliyowasilishwa ina afya njema na imeandaliwa kwa kuzingatia changamoto halisi zinazowakabili watumishi wa umma.

“Bajeti hii imegusa maeneo muhimu ikiwemo ujenzi wa majengo ya vituo vya afya, miundombinu ya barabara pamoja na stahiki za watumishi kama mafunzo na fedha za likizo. Tunatarajia changamoto nyingi kupatiwa ufumbuzi kupitia utekelezaji wake,” alisema Dkt. Njama.

Kwa ujumla, bajeti hiyo inatajwa kuwa nyenzo muhimu itakayochochea utoaji wa huduma bora kwa wananchi wa Manispaa ya Ubungo, huku ikiimarisha ustawi na motisha kwa watumishi wa umma.

Katika mwaka wa fedha 2026/2027, Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo kupitia Kamati ya Fedha na Uongozi inatarajia kukusanya na kupokea jumla ya Shilingi 149,227,080,240.00. Kati ya fedha hizo, Shilingi 53,157,960,000.00 ni mapato ya ndani, huku Shilingi 96,069,120,240.00 zikitoka Serikali Kuu na wadau wa maendeleo.

Kati ya fedha hizo za maendeleo, Shilingi 7,635,554,000.00 ni fedha za maendeleo ya ndani (Local Fund), Shilingi 6,887,310,000.00 ni fedha za nje kutoka kwa wadau wa maendeleo (Foreign Fund), Shilingi 80,847,182,240.00 ni fedha za mishahara, na Shilingi 699,074,000.00 ni fedha za matumizi mengineyo (OC). Sanjari  na hilo makisio ya matumizi ya bajeti kwa mwaka wa fedha 2026/2027

Manispaa ya Ubungo inatarajia kutumia jumla ya Shilingi 149,227,080,240.00. Kati ya fedha hizo, Shilingi 33,725,583,500.00 ni matumizi ya kawaida sawa na asilimia 23 ya bajeti, Shilingi 80,847,182,240.00 ni mishahara sawa na asilimia 54, na Shilingi 34,654,314,500.00 ni fedha za miradi ya maendeleo sawa na asilimia 23 ya bajeti yote.