SERIKALI KUNUNUA NDEGE NNE ZA BOMBARDIER KUBORESHA HUDUMA ZA ATCL
Na Hawa Ismail- Dar es Salaam
Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, ametangaza kuwa mwaka 2026 Serikali inatarajia kununua ndege nyingine nne (4) aina ya Bombardier Q400 kwa ajili ya kuboresha huduma za Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL).
Hatua hiyo ni sehemu ya mkakati wa kuimarisha usafiri wa anga nchini sambamba na utekelezaji wa ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) iliyoahidi ununuzi wa ndege nane ndani ya kipindi cha miaka mitano.
Akizungumza na waandishi wa habari Februari 26, 2026, Msigwa amesema ununuzi wa ndege hizo nne ni hatua muhimu katika kukamilisha ahadi ya CCM, huku akisisitiza kuwa lengo kuu ni kuongeza ufanisi wa ATCL, kupanua wigo wa safari za ndani na kuboresha upatikanaji wa huduma za usafiri wa anga kwa wananchi.
Wakati huohuo, wananchi wa Kimara jijini Dar es Salaam wameombwa kuwa wavumilivu kufuatia changamoto ya usafiri inayoendelea kulikumba eneo hilo, wakati Serikali ikiendelea kuchukua hatua za haraka kutatua hali hiyo.
Msigwa amesema Serikali ipo katika hatua za mwisho za kusaini makubaliano na mzabuni wa Mofat ili kumuongezea muda wa kutoa huduma ya usafiri kati ya Kimara na katikati ya jiji, hatua inayolenga kupunguza adha ya usafiri kwa wakazi wa eneo hilo katika kipindi cha mpito.
Aidha, ameeleza kuwa kampuni ya TransDar inatarajiwa kuanza kutoa huduma za usafiri katika eneo la Kimara kwa kuingiza takribani mabasi 120, hatua itakayosaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza msongamano na kuboresha usafiri kwa wananchi.


