Breaking News

Waziri Mchengerwa: Ndani ya Miaka Mitatu, Hakuna Mtanzania Atakayetibiwa Saratani Nje ya Nchi

 

Na Hawa Ismail- Dar es Salaam 

Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa, ameitaka Bodi mpya ya Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI) kuhakikisha kuwa ndani ya kipindi cha miaka mitatu, hakuna Mtanzania anayelazimika kwenda nje ya nchi kwa ajili ya matibabu ya saratani. Wito huo umetolewa kufuatia uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika vifaa tiba na miundombinu ya kisasa, hatua iliyoiweka Tanzania miongoni mwa nchi chache barani Afrika zenye huduma za kisasa za matibabu ya saratani.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa Bodi hiyo, Waziri Mchengerwa alikagua miradi mikubwa ya kimkakati inayotekelezwa na ORCI, ikiwemo ununuzi na ufungaji wa mashine tatu mpya za tiba ya mionzi (LINAC na Cobalt), mashine za uchunguzi wa kisasa kama PET CT, uanzishaji wa kinu cha kuzalisha dawa za nyuklia (Cyclotron), pamoja na ujenzi wa jengo jipya la huduma za kimataifa kwa wagonjwa wa ndani na nje ya nchi.

Waziri Mchengerwa alipongeza Menejimenti ya ORCI kwa kutekeleza agizo lake la Desemba mwaka jana la kuhakikisha mashine tatu za PET CT zilizokuwa hazijafungwa zinaanza kazi. Alieleza kuwa hadi Februari mwaka huu, mashine hizo zitakuwa tayari kutoa huduma baada ya mafundi kutoka Marekani na Ujerumani kukamilisha kazi ya ufungaji.

Katika ziara hiyo, Waziri alipata fursa ya kuzungumza na baadhi ya wagonjwa waliokuwa wakipatiwa huduma, ambapo kwa niaba yao, Bi. Justina Allen alimshukuru Rais Samia kwa kuboresha huduma za tiba ya mionzi na kuwezesha wananchi masikini kupata matibabu bure kwa kufuata utaratibu rasmi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa ORCI, Dkt. Diwani Msemo, alieleza kuwa kukamilika kwa ufungaji wa mashine hizo kutapunguza muda wa kusubiri huduma kutoka wiki 20 hadi wiki mbili pekee. Aidha, uwezo wa taasisi hiyo kuhudumia wagonjwa utaongezeka kutoka wagonjwa 200 hadi zaidi ya 400 kwa siku, hatua itakayowezesha ORCI kutoa huduma kwa wagonjwa kutoka nje ya nchi kupitia tiba ya mionzi ya kiutalii.

Waziri Mchengerwa alisisitiza kuwa mageuzi ya kweli katika huduma za saratani hayaishii kwenye majengo au vifaa, bali yanapaswa kuanzia kwenye usanifu wa utoaji huduma kwa mgonjwa na kuendelea hadi katika uzoefu wake wa kupata huduma. Alitoa wito kwa Bodi kuwa bunifu, jasiri na kuvunja mazoea ya zamani, huku akisisitiza kuwa ORCI inapaswa kuwa kielelezo cha ubunifu wa huduma za saratani barani Afrika.

“ORCI haiwezi kuwa taasisi ya kawaida. ORCI lazima iwe mamlaka ya Afrika katika saratani,” alisisitiza Waziri Mchengerwa.

Aidha, alihimiza matumizi ya teknolojia za kisasa kama mifumo ya taarifa za kitabibu (EMR) na mifumo ya kidijitali ya kupanga huduma ili kupunguza urasimu, gharama, ucheleweshaji na msongo kwa wagonjwa na familia zao.

Waziri pia alielekeza Bodi hiyo kujiwekea mifumo madhubuti ya usimamizi kupitia Kamati za Bodi kwa kuzingatia falsafa ya “eyes on, hands off”, yaani kusimamia kwa karibu bila kuingilia majukumu ya Menejimenti.

Alisisitiza kuwa lengo kuu la ORCI ni kuokoa maisha, kutoa tiba bora na kuboresha huduma kwa wagonjwa. Alitaka pia taasisi hiyo kuwekeza katika utafiti wa saratani unaotokana na huduma halisi, na kuwasilisha mpango mahsusi wa kuifanya ORCI kuwa taasisi inayoongoza kwa utafiti wa saratani barani Afrika.