Breaking News

Jeshi la Polisi Dar es Salaam Laimarisha Usalama, Watuhumiwa wa Makosa Makubwa Wahukumiwa Vifungo Vizito

 


Na Mwandishi Wetu- Dar es Salaam 

Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam, kwa kushirikiana na mamlaka nyingine za kisheria pamoja na wananchi, limeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuimarisha hali ya usalama katika maeneo tofauti ya jiji.

Hayo ameyasema leo jijini Dar es Salaam wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari leo Januari 31,2026 ambapo alisema Kipaumbele kimekuwa ni kusimamia mifumo madhubuti ya kuzuia na kudhibiti vitendo vya kihalifu ili kulinda usalama wa raia na mali zao.

"Makosa dhidi ya binadamu yameendelea kuwa chukizo kubwa kwa jamii, yakiwemo mauaji, ubakaji, ulawiti, kutorosha wanafunzi pamoja na kuwapa mimba wanafunzi. Kupitia ofisi za Mashitaka na Mahakama, Jeshi la Polisi limefanikiwa kuwachukulia hatua za kisheria watuhumiwa wa makosa hayo" alisema Kamanda Muliro 

Kati ya mwezi Desemba 2025 na Januari 2026, baadhi ya kesi zilizofikishwa mahakamani na kufikia hatua ya mwisho ziliwezesha watuhumiwa kupatikana na hatia. Miongoni mwao ni:

Peter Julius, mkazi wa Mbezi Mwisho, aliyefungwa kifungo cha maisha jela na Mahakama ya Wilaya ya Ubungo kwa kosa la ulawiti.

Dunia Sadick (Dunia), mkazi wa Chanika, aliyefungwa kifungo cha miaka 30 jela na Mahakama ya Wilaya ya Ilala kwa kosa la kubaka.

Rajab Rashid Goma, mkazi wa Mwanagati, aliyefungwa kifungo cha maisha jela na Mahakama ya Wilaya ya Ilala kwa kosa la ulawiti.

John Jacob Nyamahemba, mkazi wa Mbagala, aliyefungwa kifungo cha maisha jela na Mahakama ya Wilaya ya Temeke kwa kosa la kubaka.

Abdallah Faustin, mkazi wa Kibada, aliyefungwa kifungo cha miaka 30 jela na Mahakama ya Wilaya ya Kigamboni kwa kosa la kubaka.

Abubakar Jumanne Membe (Abuu), mkazi wa Mbagala, aliyefungwa kifungo cha maisha jela na Mahakama ya Wilaya ya Temeke kwa kosa la ulawiti.

Katika suala la usalama barabarani Kamanda Muliro alisema, Polisi Dar es Salaam imeendelea kutoa elimu kwa watumiaji wa barabara na sasa inatoa onyo kali kwa madereva wa vyombo vya moto wanaokiuka sheria za usalama barabarani. Jeshi la Polisi halitasita kuchukua hatua kali za kisheria dhidi ya madereva wazembe, wakiwemo wanaopita kwenye barabara za mabasi ya mwendokasi kinyume cha sheria.

Aidha Kamanda Muliro alisema jeshi la polisi linatambua kuwepo kwa mchezo wa kimataifa wa Ligi ya Mabingwa Afrika kwa klabu, utakaofanyika siku ya Jumapili tarehe 01 Februari 2026 saa 10:00 jioni katika Uwanja wa Benjamini Mkapa jijini Dar es Salaam, kati ya Simba SC ya Tanzania na Esperance de Tunis ya Tunisia. 

Jeshi la Polisi linawahakikishia wapenzi na mashabiki wa soka usalama wa kutosha ndani na nje ya uwanja hivyo 

Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam linawatakia kila la heri na mafanikio wawakilishi wa Tanzania, Simba SC, katika mchezo huo muhimu.