Breaking News

Simbachawene: Desemba 9 Ni Siku ya ya kusherekea sikukuu za Uhuru, Si Maandamano

 

Na Hawa Ismail- Dar es Salaam 

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene, amesema kuwa tarehe 9 Desemba 2025 ni maalum kwa ajili ya kusherehekea Uhuru wa Tanzania na si siku ya kufanya maandamano.

Ametoa kauli hiyo leo, Desemba 8, 2025 jijini Dar es Salaam akiwa kwenye mkutano na waandishi wa habari, ambapo alisisitiza umuhimu wa kulinda amani ya nchi pamoja na kuepuka vitendo vya vurugu.

“Hayo maandamano si halali kwa sababu hakuna mtu yeyote aliyewasilisha maombi ya kupata kibali. Hayajulikani yanaanzia wapi, yanaishia wapi, wala madhumuni yake ni nini,” alisema Simbachawene.

Aidha, aliwashukuru viongozi wa dini kwa kuendelea kuhubiri amani na kuhimiza umoja nchini. Aliongeza kuwa kuvuruga amani kunaweza kuathiri huduma za kijamii na hivyo alisisitiza kuwa maandamano yasiyo na ukomo ni kinyume cha sheria. Kwa mujibu wake, vyombo vya ulinzi na usalama vitaendelea kudhibiti hali ya usalama ili kuhakikisha raia na mali zao zinalindwa.

Katika hatua nyingine, Simbachawene alisema kuwa Jeshi la Polisi limetoa namba maalum kwa ajili ya kupokea taarifa mbalimbali, hatua ambayo inalenga kuboresha usalama wa wananchi na mali zao nchini.