Breaking News

Serikali Yaipeleka NIDA Kidijitali: Yazindua Namba Maalum ya SMS kwa Ufuatiliaji wa Vitambulisho vya Taifa

 

Na Hawa Ismail- Dar es Salaam 

Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi imezindua rasmi mfumo mpya wa kidijitali utakaowawezesha wananchi kufuatilia hatua za maombi ya Vitambulisho vya Taifa kwa njia rahisi na ya haraka kupitia ujumbe mfupi wa maneno (SMS).

Akizungumza leo Desemba 29, 2025 jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa huduma hiyo, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mheshimiwa George Simbachawene, ametangaza namba maalum ya SMS *15274* ambayo wananchi wataitumia kufahamu hatua iliyofikiwa katika maombi yao ya kitambulisho, ikiwa ni pamoja na kujua kama kitambulisho kimeshachapishwa au kiko tayari kuchukuliwa.

Waziri Simbachawene amesema kuwa licha ya vitambulisho vingi kuwa tayari vimezalishwa na kupelekwa katika maeneo mbalimbali ya nchi, hususan katika wilaya ambako waombaji walijiandikisha, bado kuna idadi kubwa ya wananchi ambao hawajavifuata vitambulisho hivyo. Hali hiyo imekuwa kikwazo kwa wananchi kupata huduma muhimu kama vile huduma za afya, mafao ya ustawi wa jamii, usajili wa wanafunzi vyuoni, pamoja na mikopo kutoka Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB).

“Kwa sasa, kuna vitambulisho vingi sana vilivyopo wilayani ambavyo havijachukuliwa. Sababu kubwa ni kwamba waombaji hawajui kama vitambulisho vyao vimekamilika. Kupitia mfumo huu wa 15274, mtu atajibiwa ndani ya siku tano kuhusu hali ya maombi yake, na kama hajapata, atapewa sababu,” alisema Waziri Simbachawene.

Aidha, Waziri huyo alieleza kuwa serikali inatafakari uwezekano wa kusitisha matumizi ya namba ya utambulisho (NIN) kama mbadala wa kitambulisho halisi, kwa kuwa baadhi ya watu wamekuwa wakitegemea tu namba hiyo na kuacha kuchukua vitambulisho vyao vilivyozalishwa kwa gharama kubwa kwa kutumia fedha za walipa kodi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Bw. James Kaji, alisema kuwa mamlaka hiyo imekuwa ikisambaza vitambulisho hadi ngazi ya kata, lakini bado wananchi wengi hawajavifuata. Aliongeza kuwa mfumo huu mpya wa SMS utarahisisha upatikanaji wa taarifa kwa waombaji, kwani sasa wanaweza kupata taarifa hizo moja kwa moja kupitia simu zao za mkononi.

Katika tukio hilo lililofanyika Makao Makuu ya NIDA, Waziri Simbachawene alibonyeza kitufe kuashiria uzinduzi rasmi wa huduma hiyo ya SMS. Tukio hilo pia lilihudhuriwa na Mkurugenzi Mkuu wa NIDA Zanzibar, Bw. Abdallah Mmanga, pamoja na viongozi wengine waandamizi wa serikali.

Huduma hii mpya ni sehemu ya jitihada za serikali kupeleka huduma za NIDA kidijitali, kwa lengo la kuongeza ufanisi, uwazi na kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wananchi wote nchini.