SERIKALI YAIPATIA TFS VIFAA VYA KISASA VYENYE THAMANI YA ZAIDI YA Sh. 3.2 Bilioni
Akizungumza Jijini Dodoma jana baada kukabidhi vifaa hivyo kwa Kamishna wa Uhifadhi wa TFS, Profesa Dos Santos Silayo,
Na Mwandishi wetu Dodoma
SERIKALI, kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii imeipatia Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) vifaa mbalimbali vya kisasa vyenye thamani ya zaidi ya Shilingi bilioni 3.2.
Utoaji wa vifaa hivyo unalenga kuisaidia TFS kuboresha jitihada za kuhifadhi misitu, rasilimali asili, mashamba ya miti, pamoja na kuimarisha shughuli za ulinzi wa rasilimali hizo kwa kutumia teknolojia za kisasa.
Vifaa hivyo vilivyonunuliwa na Serikali kuu ni pamoja na magari mapya 33 (Land Cruiser), pikipiki 36, na ndege nyuki (drones) za kisasa tatu.
Akizungumza Jijini Dodoma jana baada kukabidhi vifaa hivyo kwa Kamishna wa Uhifadhi wa TFS, Profesa Dos Santos Silayo, Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Ashatu Kijaji alisema utoaji wa vifaa hivyo unaakisi juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan katika kukuza sekta ya misitu na maliasili nchini Tanzania.
" Raisi Samia amekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha TFS inapata vifaa vya kisasa na vya kutosha ili kuweza kuboresha ufanisi na tija wa sekta ya misitu na maliasili," Waziri Kijaji alisema.
Dkt. Kijaji alisema sekta ya misitu inatoa mchango mkubwa sana katika kukuza pato la Taifa, na maendeleo ya kijamii nchini, hivyo Serikali ya awamu ya sita itaendelea kuchukua hatua mbalimbali kuhakikisha sekta hiyo inaendelea kuboreshwa.
Aidha, Waziri Kijaji ameutaka uongozi wa TFS kuhakikisha vitendea kazi hivyo vilivyonunuliwa na Serikali kwa gharamu kubwa vinatumika kizalendo Ili kuleta matokeo chanya.
Akizungumza baada ya kupokea vifaa hivyo, Profesa Silayo alimpongeza Rais Samia kwa kuipatia TFS vifaa hivyo ambavyo amesema vitatoa mchango mkubwa katika kuboresha utekelezaji wa majukumu yao kila siku.
“Kwa mfano, magari mapya 33 tuliyopokea yataimarisha shughuli za uhifadhi wa misitu na mashanba ya miti, pamoja na shughuli nyingine za kimsingi,” alishukuru.
Aliongeza, pikipiki 36 walizopatiwa zitawasaidia askari wa uhifadhi kufika katika maeneo ya uhifadhi ambayo hayafikiki kiurahisi kwa magari kutokana na changamoto za miundombinu ya barabara.
Pia, Profesa Silayo aliipongeza Serikali kwa kuwapatia ndege nyuki (drones) za kisasa ambazo zinaendeleza juhudi za TFS kuwekeza zaidi katika matumizi ya teknolojia za kisasa.
“Moja kati ya malengo yetu makubwa ni kuhakikisha TFS inakuwa na vifaa vinavyotumia teknolojia ya juu katika kufuatilia usalama wa misitu na katika maeneo mengine yenye maliasili," alisema.
Alibainisha kuwa katika kipindi cha mwaka huu wa fedha, Serikali imenunua na kuipatia TFS ndege nyuki kumi za kisasa.
“Hizi ndege nyuki ni za kisasa sana, na zenye uwezo wa kuruka hadi urefu wa mita 5000 juu usawa wa bahari huku zikikagua na kutoa taatifa muhimu, ikiwa ni pamoja na taatifa za uhalifu na matukio ya moto kwenye maeneo ya hifadhi,” alielezea.




