Breaking News

Meya wa Temeke Atoa Maelekezo ya Kusimamia Ahadi za Rais Ndani ya Siku 69 Zilizobaki

 

Na Hawa Ismail-Dar es Salaam 

Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Temeke, Mhe. Uzairu Abdul Athumani, ametoa maelekezo kwa Mkurugenzi na watumishi wote kuhakikisha kuwa kila mkuu wa idara anasimamia utekelezaji wa ahadi zote zilizotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ndani ya siku 69 zilizobaki katika kipindi cha siku 100 za mwanzo wa utekelezaji wa mipango ya maendeleo.

Akizungumza leo Desemba 3, 2025 jijini Dar es Salaam wakati wa kikao cha Baraza la Madiwani, Mhe. Uzairu alisisitiza umuhimu wa usimamizi madhubuti wa fedha na rasilimali watu kama nguzo kuu ya maendeleo ya Manispaa ya Temeke.


“Nimewaelekeza kuhusu usimamizi na matumizi ya miradi, hasa ile ya kimkakati, kutokana na changamoto ya kutokuwepo kwa uwiano kati ya fedha zinazotolewa na thamani ya miradi. Tumeamua kukaa pamoja, kushauriana na kuelekezana ili kuhakikisha tunawapatia wazabuni sahihi na miradi inatekelezwa kwa wakati na kwa viwango vinavyotakiwa,” alisema Mhe. Uzairu.

Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Miburani, Mhe. Rajab Mkenga, alieleza kuwa wako tayari kuanza kazi kwa bidii ili kuwatumikia wananchi na kuhakikisha maendeleo yanapatikana kwa kasi na kwa ufanisi.

 “Maagizo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan yanataka kasi. Sisi kama wasaidizi wake tunapaswa kuhakikisha kila jambo linalowagusa wananchi linashughulikiwa kwa haraka na kwa ufanisi,” alisema Mhe. Mkenga.

Katika hatua nyingine, Diwani wa Viti Maalum, Mhe. Farida Mkwanywe, aliahidi kusimamia upatikanaji wa fursa kwa wanawake na vijana, ikiwa ni pamoja na kuwawezesha wajasiriamali wadogo na kusimamia ipasavyo mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na manispaa.

Naye Diwani wa Viti Maalum, Mhe. Mwanaidi Walaji, alieleza dhamira ya kubadilisha maisha ya wanawake wa Temeke kwa kuwapelekea miradi ya maendeleo, kuwapa mafunzo na kuwaondoa kwenye utegemezi wa mikopo isiyo na tija ili waweze kujikwamua kiuchumi.

Kwa upande mwingine, mwakilishi wa wananchi, Yasini Jumanne, alieleza matumaini yake kwa baraza jipya la madiwani na uongozi wa Meya mpya, akisema kuwa Temeke inaelekea kubadilika, hasa kwa vijana kupitia wizara mpya ya vijana iliyoundwa.