Breaking News

"LUGHA YA DHARAU,KEJELI HAINA NAFASI KANISANI" LUDOVICK JOSEPH

Na Mwandishi Wetu- Dar es Salaam 

Upinzani wa waumini wa Kanisa Katoliki dhidi ya mwenendo wa baadhi ya viongozi wa juu wa Kanisa, akiwemo Padri Dkt. Charles Kitima na Askofu Mkuu Jude Thaddaeus Ruwa’ichi, unaendelea kushika kasi. Hoja mbalimbali za kimaadili, kisheria na kiteolojia zimeanza kutolewa hadharani, zikilenga kuhoji nafasi na mienendo ya viongozi hao ndani ya Kanisa.

Kupitia tafakuri nzito ya dhamiri iliyotolewa na Mwalimu Ludovick Joseph, mmoja wa waumini wa Kanisa Katoliki nchini Tanzania, waumini wameanza kujenga msimamo wa pamoja kwamba Kanisa si mtu mmoja, si padri wala askofu, bali ni jumuiya ya waamini. Wanasema kuwa viongozi wa Kanisa hawako juu ya Injili, wala juu ya waumini wanaowahudumia.

Katika tafakuri hiyo, waumini wanasisitiza kuwa kuhoji, kukosoa au kuomba uchunguzi dhidi ya kiongozi wa Kanisa si uasi, si dhambi, wala si chuki, bali ni haki ya msingi inayotambuliwa ndani ya sheria ya Kanisa Katoliki (Canon Law).

 “Kanisa ni takatifu kwa sababu ya Kristo, lakini viongozi wake ni wanadamu wenye mipaka na wanaweza kukosea,” inasomeka sehemu ya tafakuri hiyo, ikisisitiza kuwa hakuna kiongozi aliye juu ya Injili. Alisisitiza Ludovick

Waumini wameeleza wasiwasi mkubwa kuhusu matumizi ya lugha ya dharau, kejeli na matusi kutoka kwa baadhi ya viongozi wa Kanisa dhidi ya waamini. Wanasema madhabahu si jukwaa la jazba wala fedheha, bali ni mahali pa kufundisha, kuponya na kuijenga jamii ya waamini kwa upendo na hekima.

Kwa kunukuu Maandiko Matakatifu, tafakuri hiyo inabainisha kuwa lugha ya dharau haina nafasi katika mafundisho ya Kikristo. Kiongozi wa kiroho anatakiwa kuhubiri kwa unyenyekevu, kwa neema, na kwa kuzingatia heshima ya waumini wote.

Kwa msisitizo mkubwa, waumini wanakumbusha mafundisho ya Injili yanayolitaka Kanisa kujitathmini na kujirekebisha lenyewe kabla ya kuikosoa jamii au Taifa.

Tafakuri hiyo inanukuu Mathayo 7:3–5 kuhusu kuondoa “boriti” katika jicho la mtu mwenyewe kabla ya kuona “kibanzi” katika jicho la mwingine.

Hoja hii inaelezwa kuwa ndiyo msingi wa maadili unaolipa Kanisa uhalali wa kutoa sauti ya kinabii dhidi ya maovu ya dunia.

Tafakuri hiyo pia inaibua hoja nzito kuhusu kuingizwa kwa Kanisa katika siasa za vyama. Inatahadharisha kuwa hatua hiyo:

- Huwagawa waumini,

- Huporomosha mamlaka ya kimaadili ya Kanisa,

- Huhatarisha umoja wa Kanisa na Taifa.

Kwa mantiki hiyo, waumini wanasema kuwa hatua za baadhi ya viongozi wa Kanisa kujihusisha au kuonekana kujihusisha na siasa za vyama ni kosa la kimaadili linalopaswa kutafakariwa kwa kina na kurekebishwa kwa haraka.

Katika kile kinachoonekana kama msimamo unaozidi kuimarika, waumini wanaunga mkono hatua ya kuwasilisha barua kwa Balozi wa Vatican (Nunsio) nchini Tanzania, wakitaka uchunguzi wa mwenendo wa Padri Dkt. Charles Kitima.

Wanasema hatua hiyo:

- Iko ndani ya sheria ya Kanisa (Canon Law),

- Inalenga kulinda heshima na hadhi ya Kanisa,

- Si uasi, bali ni wajibu wa Kikristo wa uwajibikaji.

Tafakuri hiyo inahitimisha kwa ujumbe mzito kwa uongozi wa Kanisa Katoliki nchini Tanzania kwamba mamlaka ya kiroho ni huduma, si utawala.

 “Kulilinda Kanisa ni kulinda ukweli, si kulinda makosa ya mtu,” waumini wanasema, wakikumbusha kuwa mwili wa Kristo una viungo vingi, na kila muumini ana haki na wajibu wa kulilinda Kanisa lake kwa ujasiri, upendo na ukweli.