Breaking News

Wanawake Wapaza Sauti: Wito wa Ushiriki wa Kijinsia Katika Uchaguzi Mkuu wa 2025

 

Muunganiko wa Asasi za wanawake kuelekea uchaguzi mkuu 

Na Hawa Ismail – Dar es Salaam

Kadri Watanzania wanavyojiandaa kushiriki Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 29, 2025, muungano wa asasi za wanawake na watetezi wa usawa wa kijinsia umeibuka na tamko lenye msisitizo kwa wananchi kuhakikisha wanawake wanashiriki kikamilifu katika siasa, uongozi na upigaji kura.

Kwa mujibu wa tamko hilo lililotolewa na waasisi wa asasi za kiraia ambalo limesomwa  na  Rose Haji Mwalimu kutoka TAMWA leo jijini Dar es Salaam, asasi hizo zinasisitiza kuwa huu ni wakati wa taifa kuthibitisha kuwa uongozi bora haupimwi kwa misingi ya jinsia, bali kwa uwezo, maadili na dhamira ya kweli ya kuwatumikia wananchi.

Muungano huo umeeleza kuwa ushiriki wa wanawake katika siasa ni msingi muhimu wa kukuza demokrasia jumuishi na kuhakikisha masuala ya kijinsia, uchumi na maendeleo ya jamii yanapewa kipaumbele.

“Tunawahimiza wanawake wote kujitokeza kwa wingi kupiga kura Oktoba 29. Ni fursa ya kuchagua viongozi watakaosimamia ajenda za maendeleo zinazogusa maisha ya wanawake na watoto,” alisema Rose Mwalimu 

Aidha kwa upande wake Na Lucy Kilasi kutoka shirika women welfare tz amesema mwaka huu Tanzania imepiga hatua kubwa katika usawa wa kijinsia kisiasa, ambapo Rais Samia Suluhu Hassan anawania tena urais kupitia CCM. Aidha, wanawake wengine wawili — Saumu Rashid (UDP) na Mwajuma Mirambo (UMD) — wamejitokeza kuwania urais, huku vyama vingi vikiongeza idadi ya wagombea wenza wanawake.

“Hii ni hatua muhimu katika historia ya siasa ya Tanzania. Inaonesha kuwa jamii inaanza kuamini uwezo wa mwanamke kushika nafasi za juu za uongozi,” limeeleza tamko hilo. Alisema Lucy Kilasi 

Pia Lucy Kilasi alisema Asasi hizo zimekemea vikali vitendo vya kejeli, udhalilishaji na mashambulizi ya kibinafsi dhidi ya wanawake wanasiasa, zikieleza kuwa vitendo hivyo vinadhoofisha motisha na ushiriki wa wanawake katika siasa.

“Mwanamke kiongozi asihukumiwe kwa jinsia yake, bali kwa uwezo na dira yake ya maendeleo. Uongozi wa mwanamke si tishio, ni fursa ya demokrasia jumuishi,” alisema Lucy Kilasi

Muungano huo umeitaka Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kuhakikisha uchaguzi unafanyika katika mazingira salama, huru na yasiyo na vitisho vya kijinsia. Pia, vyombo vya habari vimetakiwa kutoa nafasi sawa kwa wagombea wanawake na kuratibu mijadala inayojenga uelewa wa umma kuhusu mchango wa wanawake katika maendeleo ya taifa.

Asasi hizo zimepongeza uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendeleza ajenda ya usawa wa kijinsia kupitia utekelezaji wa Dira ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa (SDG 5). Taarifa hiyo imeeleza kuwa mageuzi ya kisheria na miradi mikubwa ya maendeleo katika sekta za afya, elimu na uwezeshaji wa wanawake kiuchumi ni ushahidi wa dhamira hiyo.

Tamko hilo limehitimisha kwa kusisitiza kuwa maendeleo ya taifa hayawezi kupatikana bila ushiriki sawa wa wanawake na wanaume katika maamuzi. “Uongozi bora hauna jinsia — una maadili, dira na dhamira ya dhati ya kuwatumikia wananchi. Tanzania ni yetu sote, na kila mmoja ana wajibu wa kuchangia katika kuijenga,” limeeleza.