Breaking News

Urusi na Tanzania Zaendeleza Ushirikiano Katika Elimu ya Juu

 

Na Hawa Ismail- Dar es Salaam 

Mwakilishi wa Naibu Katibu Mkuu kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Bw. Clement Sanga, amesema kuwa ushirikiano wa kielimu kati ya Tanzania na Urusi unaimarisha mahusiano ya kimataifa na kufungua milango ya kubadilishana wahadhiri na wanafunzi kati ya nchi hizo mbili.

Akizungumza katika maonyesho ya elimu yaliyoandaliwa na Kituo cha Sayansi na Utamaduni cha Urusi jijini Dar es Salaam, Bw. Sanga alieleza kuwa tukio hilo limewaleta pamoja wawakilishi kutoka vyuo 12 vya Urusi, ikiwa ni ongezeko kutoka vyuo 10 vilivyoshiriki mwaka uliopita. Maonyesho hayo yalilenga kutoa fursa kwa Watanzania kuomba ufadhili wa masomo (scholarship) nchini Urusi.

Bw. Sanga alisisitiza kuwa ushirikiano huu umechangia ongezeko la wanafunzi wa kimataifa wanaojifunza lugha ya Kiswahili, hasa barani Afrika. Aliongeza kuwa mtaala mpya wa elimu nchini Tanzania unahimiza kujifunza lugha mbalimbali, hivyo Watanzania wana nafasi ya kujifunza Kirusi katika shule za sekondari na vyuo vikuu. “Ujuzi wa lugha ya kigeni huchochea uelewa wa tamaduni na huimarisha sekta ya utalii. Hii huchangia ongezeko la watalii wanaotembelea nchi yetu,” alisema Bw. Sanga.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kituo cha Urusi cha Sayansi na Utamaduni, Bw. Alexander Evstigneev, alieleza furaha yake kuona idadi ya wanafunzi wanaopata nafasi ya kusomea Urusi ikiongezeka kutoka 90 hadi 150, ambapo 50 kati yao watajikita katika masomo ya sayansi.

Mwanafunzi kutoka Chuo cha Afya Excellent, Twaha Shabani Abdallah, alieleza kufurahishwa na maonyesho hayo, akisema yalimpa mwanga kuhusu vyuo vya Urusi na kumvutia kusomea udaktari. Alihimiza vijana wenzake kuchangamkia fursa hizo ili kuimarisha mahusiano kati ya Tanzania na Urusi.

Naye Anna Lucas Simba, mmoja wa wahitimu waliomaliza masomo ya famasi katika Chuo cha Michael States University nchini Urusi, alieleza kuridhishwa na ubora wa elimu ya vitendo pamoja na fursa ya kujifunza lugha na utamaduni wa Kirusi.