Breaking News

WATAALAMU WA MOYO WATANGAZA TAHADHARI: MTINDO WA MAISHA UNACHANGIA KUONGEZEKA KWA MAGONJWA YA MOYO TANZANIA



Na Mwandishi Wetu NICOMEDIADIGITAL 

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Dkt. Peter Kisenge, ameeleza kuwa ongezeko la magonjwa ya moyo nchini Tanzania linachangiwa na sababu zinazozuilika, hasa mtindo wa maisha usiozingatia afya. Amezitaja sababu hizo kuwa ni pamoja na kutofanya mazoezi, uvutaji wa sigara kupita kiasi, unywaji wa pombe uliokithiri, na ulaji wa vyakula visivyozingatia lishe bora—hususan vyenye mafuta mengi, wanga kupita kiasi bila mazoezi, na protini nyingi kutoka kwa wanyama kama ng’ombe, mbuzi na kondoo.

Aidha, Dkt. Kisenge alisisitiza umuhimu wa wajawazito kujiepusha na matumizi ya pombe, sigara, na dawa bila ushauri wa daktari katika miezi sita ya mwanzo ya ujauzito. Pia alihimiza ulaji wa vyakula vyenye foliki asidi na udhibiti wa kisukari wakati wa ujauzito ili kuepuka matatizo ya kiafya kwa mtoto anayezaliwa.


“Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete inaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu namna ya kujikinga na magonjwa ya moyo kwa kufanya mazoezi angalau nusu saa mara tatu kwa wiki, pamoja na kufuatilia afya zao kwa kupima shinikizo la damu, kiwango cha sukari na kolesteroli,” alieleza Dkt. Kisenge.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa JKCI na daktari bingwa wa magonjwa ya moyo, Dkt. Tulizo Shemu Sanga, alieleza kuwa magonjwa ya moyo yanaathiri uchumi kwa kiasi kikubwa. Akizungumza jijini Dar es Salaam wakati wa maadhimisho ya Siku ya Moyo Duniani, yenye kauli mbiu “Don't Miss a Beat,” Dkt. Tulizo alisema kuwa zaidi ya asilimia 60 hadi 70 ya vifo vinavyotokana na maradhi yanahusiana na moyo, hali inayosababisha watu kushindwa kutekeleza majukumu yao ya msingi.

Aliongeza kuwa kutoshughulikia matatizo ya shinikizo la damu mapema kunaweza kusababisha uharibifu wa figo, ambapo gharama ya kusafisha figo kwa wiki moja ni zaidi ya shilingi milioni moja. Aidha, matibabu ya kuzibua mshipa wa moyo hugharimu hadi shilingi milioni sita, kifaa cha kusaidia umeme wa moyo hugharimu shilingi milioni kumi, na kifaa cha kusaidia moyo kufanya kazi kikamilifu hugharimu hadi shilingi milioni thelathini.

Dkt. Eva Wakuganda, daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto, alieleza kuwa katika maadhimisho hayo wameweza kupima watoto zaidi ya 25 na kugundua baadhi yao wana matatizo ya moyo ya kuzaliwa. Alitoa wito kwa wazazi kuhakikisha watoto wanapimwa mapema ili kupata matibabu stahiki na kuepuka madhara makubwa ya kiafya.

Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete imekuwa ikitekeleza kampeni ya “Tiba Mkoba” chini ya mpango wa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kusambaza huduma za afya na madaktari katika mikoa mbalimbali. Mpaka sasa, taasisi hiyo imefikia mikoa 20 nchini Tanzania, ikitoa elimu na huduma za matibabu ya moyo kwa wananchi.