TLP YAZINDUA KAMPENI KITAIFA: RWAMUGIRA AAHIDI NEEMA KWA WANANCHI
Mgombea urais wa TLP Yustas Rwamugira azindua kampeni jijini Dar es Salaam, aahidi elimu na afya bure, utawala bora na neema kwa wakulima, wajasiriamali na wananchi wote.
Na Mwandishi wetu - Dar es Salaam
Mgombea wa Urais kupitia chama cha Tanzania Labor Party (TLP), Yustas Mbatina Rwamugira, ameanza rasmi kampeni zake za kitaifa akishirikiana na mgombea mwenza wake, Bi. Amana Suleiman Mzee. Uzinduzi huo umefanyika katika viwanja vya Manzese jijini Dar es Salaam, ambapo pia waliwatambulisha wagombea wa ubunge na udiwani watakaowania nafasi mbalimbali kupitia chama hicho.
Rwamugira ameahidi kuwa serikali ya TLP itahakikisha utawala bora, usimamizi sahihi wa rasilimali na mapambano dhidi ya umaskini. Amesisitiza kuwa nchi yenye watu milioni 70 pamoja na utajiri wa madini, gesi na ardhi haiwezi kushindwa kuwapatia wananchi wake milo mitatu kwa siku. Miongoni mwa sera zake ni kuimarisha kilimo cha umwagiliaji, kuanzisha viwanda vidogo katika kila wilaya, pamoja na kutoa fursa kwa vijana wa bodaboda na bajaji kumiliki vyombo vyao bila gharama kubwa.
Aidha, Rwamugira ameahidi huduma za kijamii bure ikiwemo elimu kuanzia chekechea hadi vyuo vikuu, na mafunzo ya ufundi kwa vitendo katika sekta za kilimo, ujenzi na afya. Aliongeza kuwa serikali yake itahakikisha bima ya afya kwa kila Mtanzania na kuondoa ada zinazotozwa hospitalini kwa ajili ya kuondoa miili ya marehemu.
Awali, Mwenyekiti wa TLP Taifa ambaye pia ni mgombea ubunge wa Vunjo, Richadi Shedrak Lymo, aliwaeleza wananchi kuwa chama chake kimejipanga kubadilisha Tanzania kwa kuimarisha uchumi kupitia sera za kilimo na uwekezaji. Alisisitiza kuwa TLP ikishika dola itaweka kipaumbele katika amani ya taifa na kuhakikisha wawekezaji wageni wanalipa kodi ya haki itakayonufaisha wananchi.
Katika hatua nyingine, Lymo aliwataka vyama vya upinzani hususan CHADEMA kuungana na TLP badala ya kususia uchaguzi, akisisitiza mshikamano wa kisiasa kwa maendeleo ya taifa. TLP imepanga kushiriki uchaguzi kwa kusimamisha wagombea wa ubunge 11 akiwemo Godwin Mashota (Kisarawe), Mohammed Shabni (Temeke), Fredi Nashoni (Kinondoni), Janeth Mhando (Kivule), Nuru Mwangila (Ilala) na wengineo.
