Norway yaongeza nguvu LHRC: Ushirikiano Mpya kwa Demokrasia na Haki za Binadamu Tanzania
![]() |
| Balozi wa Norway Tone Tinnes na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Fulgence Massawe wakitia saini mkataba mpya jijini Dar es Salaam |
Na Mwandishi Wetu
Ubalozi wa Norway umesaini mkataba mpya wa miaka mitatu na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) leo tarehe 8 Septemba 2025 jijini Dar es Salaam. Kupitia mkataba huu, Norway itasaidia LHRC kwa zaidi ya shilingi bilioni 7 ili kuendeleza kazi za kutetea haki na demokrasia kwa Watanzania.
Balozi wa Norway nchini, Bi. Tone Tinnes, amesema “Makubaliano haya yanaonyesha dhamira ya muda mrefu ya Norway katika haki za binadamu nchini Tanzania. Kwa kuunga mkono LHRC, tunachangia jamii yenye haki za kisiasa, maridhiano, uwezeshaji wa wanawake na uhuru wa kujieleza, ambayo ndiyo msingi wa maendeleo ya kijamii na kiuchumi.”
Ameongeza pia kuwa mashirika ya kiraia yana nafasi muhimu sana,
“Haki za kisiasa na maridhiano ni msingi wa imani na utulivu. Demokrasia imara inategemea uhuru wa kujieleza na sauti huru, na Norway inajivunia kuunga mkono kazi za LHRC kulinda thamani hizi.”
Kwa upande wa LHRC, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Fulgence Massawe amesema msaada huu umekuwa msaada mkubwa kwa jamii,
“Ushirikiano huu umetuwezesha kusikika kwa niaba ya wanyonge, kushawishi mageuzi ya sera na kukuza jamii jumuishi na yenye usawa. Tunashukuru sana kwa dhamira ya Norway katika haki na heshima kwa wote.”
Kupitia msaada huu, LHRC itaendelea kushughulikia mageuzi ya kisheria, masuala ya uchaguzi, haki za wanawake na watoto, pamoja na kutoa msaada wa kisheria kwa wananchi.
