Breaking News

*Mtihani wa Kumaliza Elimu ya Msingi Kuanza Rasmi Kesho Tanzania*

 

Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA) limetangaza rasmi kuanza kwa Mtihani wa Kumaliza Elimu ya Msingi, utakaofanyika tarehe 10 na 11 Septemba katika maeneo mbalimbali nchini Tanzania.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Katibu Mtendaji wa NECTA, Profesa Said Mohamed, amesema jumla ya watahiniwa _1,172,279_ wamesajiliwa kushiriki mtihani huo. Kati yao, wavulana ni _535,138_ (asilimia _45.65_) na wasichana ni _637,141_ (asilimia _54.35_).

“Asilimia 93.35 ya watahiniwa watafanya mtihani kwa lugha ya Kiswahili, huku asilimia 6.65 wakitarajiwa kutumia lugha ya Kiingereza, kulingana na lugha ya kujifunzia katika shule zao,” amesema Prof. Mohamed.

Aidha, watahiniwa _4,679_ wenye mahitaji maalum wamesajiliwa, wakiwemo:

- Wasioona: _92_

- Wenye uoni hafifu: _1,551_

- Wenye uziwi: _1,079_

- Wenye ulemavu wa akili: _448_

- Wenye ulemavu wa viungo: _1,509_

Profesa Mohamed ameeleza kuwa maandalizi yote muhimu yamekamilika, yakiwemo usambazaji wa karatasi za mitihani, nyaraka muhimu, na vifaa maalum kwa ajili ya watahiniwa wenye mahitaji maalum.

Katika hatua nyingine, NECTA imetoa wito kwa jamii, wamiliki wa shule, kamati za mitihani, na wasimamizi kuhakikisha mazingira ya mtihani yanakuwa salama, tulivu, na huru dhidi ya vitendo vya udanganyifu.

“Tunawasihi wamiliki wa shule na wakuu wa shule kutojihusisha kwa namna yoyote na usimamizi wa mitihani. Baraza halitasita kuchukua hatua kali, ikiwemo kufuta kituo cha mtihani, endapo kitabainika kuhatarisha uhalali wa mtihani,” amesisitiza Prof. Mohamed.