Breaking News

Mgombea Urais wa chama cha TLP Aahidi Mageuzi Makubwa ya Kijamii na Kiuchumi

 

Mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia chama cha Tanzania Labour Party (TLP), _Yustas Mbatina Rwamugira_, ameahidi kusimamia utawala bora endapo atapata nafasi ya kuiongoza nchi. Akizungumza katika mkutano wa kampeni, Rwamugira alieleza kuwa serikali yake itahakikisha elimu inatolewa bure kuanzia ngazi ya chekechea hadi chuo kikuu.

 “Tukipata kuongoza nchi hii, tutaondoa kabisa suala la mikopo ya elimu. Tutahakikisha wanafunzi wanajifunza kwa kina—katika nadharia na ufundi—ili wanapohitimu wawe wataalamu wanaojitegemea,” alisema Rwamugira.


Rwamugira pia aliahidi kusimamia sekta ya madini kwa uwazi na ufanisi, sambamba na kuimarisha kilimo cha umwagiliaji ili kuongeza tija. Alieleza kuwa kila wilaya nchini itaanzishiwa viwanda vidogo vidogo, na bodaboda wote watawezeshwa kumiliki pikipiki zao binafsi. Aidha, alisisitiza umuhimu wa kuweka fedha benki na kugawana faida kila mwisho wa mwezi.

Katika sekta ya afya, Rwamugira aliahidi kuweka utaratibu utakaowezesha kila Mtanzania kupata bima ya afya bila ubaguzi pamoja na kutoa kutoa mwili wa marehemu hospitali bila ya malipo yoyote.

Akigusia migogoro ya wakulima na wafugaji, Rwamugira aliahidi kutatua migogoro hiyo kwa kuzikabidhi tenda zote kwa wazawa na kuhakikisha malipo kwa wote wanaoidai serikali. Pia alieleza kuwa wajasiriamali watawekewa benki zao maalum na kupewa mikopo halali isiyowaumiza.

Mwenyekiti wa TLP na mgombea ubunge jimbo la vunjo, _Richard Shedrack Lyimo_, akizungumza katika mkutano wa kampeni uliofanyika Kigamboni, aliahidi kulinda amani ya nchi na kuhakikisha Watanzania wanapata ajira kupitia uanzishaji wa viwanda vidogo.

 “Tutahakikisha wawekezaji wa ndani wanamiliki angalau nusu ya uwekezaji na kufaidika na ardhi yao. Pia kutakuwa na mchakato wa marekebisho ya katiba mpya, si suala la kukurupuka bali linahitaji maandalizi ya kina,” alisema Lyimo.

Lyimo aliongeza kuwa udalali wa pembejeo utaondolewa na wakulima watapatiwa pembejeo mapema. Alisisitiza matumizi ya teknolojia ya kisasa na kuwahamasisha wasomi kurudi vijijini ili kuendeleza kilimo chenye manufaa.

Kwa upande wake, mgombea ubunge wa Jimbo la Kigamboni, _David Michael_, aliahidi kuondoa ushuru kwenye Daraja la Kigamboni, kurejesha vivuko vilivyositishwa, na kuanzisha viwanda vidogo. Pia aliahidi kuwajengea wamachinga vibanda vyenye matairi, kujenga barabara za lami katika mitaa, na kuanzisha Saccos kwa wafanyabiashara wadogo na mama ntilie.