*Mgombea Ubunge CUF jimbo la mbagala Aahidi kuondoa ushuru kwa wafanya biashara*
Mgombea ubunge jimbo la Mbagala kupita chama cha CUF Said Kinyogori
Mgombea wa nafasi ya ubunge katika Jimbo la Mbagala kupitia Chama cha Wananchi (CUF), Said Kinyogori, ameahidi kushughulikia changamoto zinazowakabili wafanyabiashara wa eneo hilo pamoja na kuboresha huduma za afya endapo atachaguliwa.
Akizungumza leo, Septemba 11, 2025, katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye viwanja vya Zakhem jijini Dar es Salaam, Kinyogori alieleza dhamira yake ya kuleta mabadiliko chanya kwa wakazi wa Mbagala.
“Nikipata nafasi ya kuwa Mbunge wa Mbagala, nitahakikisha huduma za afya zinaboreshwa kwa kiwango cha juu. Mojawapo ya hatua nitakazochukua ni kuandaa semina kwa wauguzi na madaktari ili kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wananchi,” alisema Kinyogori.
Mbali na sekta ya afya, Kinyogori alieleza kuwa atapambana kuondoa ushuru usio wa lazima kwa wafanyabiashara wadogo na wa kati katika jimbo hilo, ili kuwapa fursa ya kukuza mitaji na biashara zao.
Kwa upande wa vijana, aliahidi kutoa elimu juu ya umuhimu wa miundombinu rafiki kwa maendeleo yao, akisisitiza kuwa uwekezaji katika rasilimali watu ni msingi wa ustawi wa taifa.


