Breaking News

JWT PWANI YAIPONGEZA SERIKALI KWA KUANZISHWA KWA TOST

 


Mwandishi wetu , pwani 


Jumuiya ya wafanyabiashara Mkoa wa pwani imeipongeza serikali ya awamu ya sita kwa Kuanzishwa kwa Taasisi ya usuluhishi wa malalamiko na taarifa za kikodi (TOST) iliyoko chini ya Wizara ya Fedha ambapo hadi kufikia Novemba, 2024 malalamiko 238 yalipokelewa na kusajiliwa na kati ya hayo, malalamiko 215 yalifanyiwa kazi na kutolewa maamuzi.

Hayo amebainisha Makamu mwenyekiti wa Jumuiya hiyo Athumani Saidi wakati akizungumza na waandishi wa habari Mkoani Pwani huku akieleza kuwa Kupunguzwa kwa migogoro isiyo ya lazima baina ya wafanyabiashara wa maduka na Wamachinga  yameleta Ufanisi mkubwa wa kibiashara Katika Mkoa huo.


Amesema kuwa serikali kupitia TRA kwa sasa wanashirikiana vizuri na wafanyabiashara katika ulipaji kodi kwa utaratibu mzuri bila ya bughudha tofauti na ilivyokuwa zamani ambapo ilifikia hatua wafanyabiashara walikuwa wakifunga maduka na kukimbia.

Amesema kuwa zamani ilifikia hatua ya kufungiwa maduka kwa kushindwa kulipa kodi lakini kwa sasa hata kama mfanyabiashara kashindwa kulipa kodi wanakaa mezani na anapewa muda wa kueleza atalipa kwa njia gani au kwa muda fulani atakapokuwa amepata fedha.

"Ukusanyaji kodi kwa sasa umekuwa ni rafiki siyo wa kubughudi wafanyabiashara bali ni kwa kushirikiana hali ambayo inawafanya wafanyabiashara kulipa kodi bila ya usumbufu,"amesema Said.

Naye mwenyekiti wa Soko la Loliondo Mohamed Mnembwe amesema kuwa wanamshukuru Rais Dk Samia Suluhu Hassan kwa kuweka mazingira mazuri ya kibiashara.

Mnembwe amesema kuwa kauli aliyoitoa Rais ya kutaka wafanyabiashara wasibughudhiwe imewafanya wafanye biashara zao bila ya changamoto hivyo kuleta mabadiliko makubwa ya kiuchumi.

Kwa upande wake Steven Shehiza  ameomba serikali itanue wigo kwa wafanyabiashara wa ndani waweze kufanyabiashara nje ya nchi ili kuongeza pato la Taifa.