Wanufaika wa Bima Wafikia Milioni 25.9: TIRA Yatoa heko kwa serikali
Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) imetangaza ongezeko kubwa la wanufaika wa huduma za bima nchini, kutoka milioni 14 mwaka 2021 hadi kufikia milioni 25.9 mwaka 2025. TIRA imesema mafanikio hayo yanatokana na juhudi za kuhamasisha wananchi pamoja na utekelezaji madhubuti wa sera za serikali.
Akizungumza Agosti 18, 2025 jijini Dar es Salaam katika kikao kazi kilichoandaliwa kwa ushirikiano na Ofisi ya Msajili wa Hazina (TR), Kamishna wa TIRA, Dkt. Baghayo Saqware, alieleza kuwa soko la bima limeimarika kwa kasi, huku mali na mitaji ikiongezeka kutoka shilingi trilioni 1.2 mwaka 2021 hadi trilioni 2.3 mwaka huu.
“Mafanikio haya yanatokana na utekelezaji mzuri wa sera chini ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan. Takwimu hizi zinaonyesha maendeleo ya kweli katika sekta ya bima,” alisema Dkt. Saqware.
Dkt. Saqware alibainisha kuwa idadi ya watoa huduma za bima imeongezeka kutoka 993 mwaka 2021 hadi 2,425 mwaka 2025, huku huduma mpya zikijumuisha bima ya afya, kidijitali, na bima mtawanyo ambayo imeongezeka kutoka kampuni moja hadi nne.
Aidha, kampuni za bima zimeongezeka kutoka 32 hadi 35, jambo linaloashiria kuvutia kwa mazingira ya uwekezaji nchini.
Serikali pia imefanikiwa kutunga Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote ya mwaka 2023 pamoja na kanuni zake, ambayo inalenga kuongeza upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi na kuweka Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) chini ya usimamizi wa TIRA.
“Sheria hii itaboresha maisha ya wananchi kwa kuwapatia huduma sahihi za afya kupitia kadi za bima, na kuongeza idadi ya watumiaji wa huduma hizo,” aliongeza Dkt. Saqware.
Katika juhudi za kulinda miradi ya serikali, Sheria ya Fedha ya mwaka 2022 imefanyiwa maboresho ili kuhakikisha miradi yote inakatiwa bima. Vilevile, TIRA imeanzisha consortium ya kilimo yenye kampuni 15, na consortium ya mafuta na gesi yenye kampuni 22, kwa lengo la kushiriki kikamilifu katika uchumi wa rasilimali hizo.
Dkt. Saqware pia alieleza mafanikio ya kuimarisha mifumo ya TEHAMA kwa kuunganisha TIRA na taasisi mbalimbali ikiwemo Benki Kuu ya Tanzania, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), LATRA, TASAC, na NIDA.
"Matarajio yetu ni kuunganisha taasisi zaidi ya 30 bara na visiwani ili kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wananchi,” alihitimisha.
