UCHAGUZI UPO, JIANDAENI KUPIGA KURA – JAJI MSTAAFU MUTUNGI
Na Kelvin Kijo, Dar es Salaam
Watanzania wametakiwa kujiandaa kikamilifu kushiriki uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika tarehe 29 Oktoba 2025, huku amani na mshikamano vikisisitizwa kuwa nguzo kuu katika kipindi cha kampeni.
Akizungumza katika mafunzo kuhusu Sheria ya Gharama za Uchaguzi yaliyofanyika leo Agosti 18, 2025 katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Mwl. Nyerere (JNICC), Jaji Mstaafu Francis Mutungi amewataka viongozi wa vyama vya siasa kuwa mabalozi wa amani na kuepuka maneno ya kuchochea mgawanyiko wa kijamii.
“Sisi viongozi lazima tuwe mfano siku zote. Kwenye mitandao mtaambiwa uchaguzi haupo, lakini mimi nasema uchaguzi upo palepale. Wakati wa kampeni acheni sera za vyama vyenu ziongee. Umoja na amani viwe kipaumbele chetu,” amesema Jaji Mutungi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Sehemu ya Ruzuku, Bw. Edmund Mugash, alifafanua kuwa Sheria ya Gharama za Uchaguzi Sura ya 278, iliyopitishwa Februari 11, 2010 na kutiwa saini na Rais Mstaafu Jakaya Mrisho Kikwete Machi 17, 2010, ililenga kuimarisha demokrasia, kudhibiti matumizi ya fedha na kuzuia vitendo vya rushwa wakati wa uchaguzi.
“Sheria hii inataka uwazi wa mapato na matumizi. Wagombea wa urais na ubunge watawasilisha taarifa kwa Tume Huru ya Uchaguzi (INEC) kwa kutumia fomu namba EE1 na EE2, huku wagombea wa udiwani wakitoa taarifa kwa kata husika,” amesema Bw. Mugash.
Aidha, alieleza kuwa kifungu cha 4 cha sheria hiyo kinampa Msajili mamlaka ya kuchunguza ukiukwaji wowote na kuwasilisha taarifa kwa INEC ili hatua stahiki zichukuliwe.
Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Prof. Ibrahim Lipumba, ameiomba Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kutafsiri sheria hiyo kwa Kiswahili ili kuwasaidia wagombea wasioelewa Kiingereza.
Naye Mwenyekiti wa Tanzania Labor Party (TLP), Ndugu Richard Shadrach Lymo, aliwataka wagombea wote kuzingatia sheria hiyo akibainisha kuwa uwajibikaji utasaidia kudhibiti mianya ya rushwa. Pia aliiomba Ofisi ya Msajili kuhakikisha fedha za ruzuku zinasambazwa kwa wakati ili elimu ifikie ngazi ya kata.
Kwa upande wa wanawake, Rosemary Justin, Katibu wa UWT Wilaya ya Ilala akimwakilisha Katibu Mkuu wa UWT Taifa, Susan Peter Kunambi, alisisitiza umuhimu wa heshima kwa wanawake wanaogombea nafasi mbalimbali.
“Natamani wanawake wanaogombea waheshimiwe kuanzia ngazi ya urais, ubunge hadi udiwani. Ushiriki wao ni muhimu katika kuimarisha demokrasia yetu,” alisema.
Katika maelezo yake mgombea urais kupitia chama cha siasa National League for Democracy (NLD) Doyo Hassan Doyo amesema amefurahishwa na usawa utaopatikana wakati wa uchaguzi kutokana na sheria hio ya Gharama za Uchaguzi.
"sheria hii inaenda kuweka usawa kwa watu ambao wana fedha nyingi zisizojulikana zimetoka wapi wakizitumia kujiweka madarakani badala ya kuwekwa na wapigakura, changamoto moja tu katika sheria hio ni kuangalia namna ya kuitafsiri kwenda lugha ya kiswahili ili hata viongozi wa udiwani waweze kuelewa vyema." amesema Doyo.
Mafunzo haya yamekusudia kuwajengea viongozi wa vyama vya siasa uelewa wa pamoja kuhusu Sheria ya Gharama za Uchaguzi, ili kuhakikisha uchaguzi wa Oktoba unafanyika kwa uwazi, haki na kwa kuzingatia misingi ya amani na mshikamano wa kitaifa.


