Mpina: "Nimegombea Urais Kupinga Mikataba Mibovu na Kutetea Maslahi ya Taifa"
Mgombea urais kwa tiketi ya ACT-Wazalendo, Luhaga Mpina, amesema ameamua kuwania nafasi hiyo ya juu ya uongozi ili kupinga mikataba mibovu, kukataa bima zinazochagua magonjwa, kutetea ajira kwa vijana, na kwa sababu yeye ni mzalendo wa kweli kwa nchi yake.
Akizungumza leo Agosti 14, 2025 jijini Dar es Salaam na waandishi wa habari pamoja na wahariri wa vyombo vya habari, Mpina alisisitiza kuwa hatua yake ya kugombea urais si maigizo bali ni dhamira ya dhati ya kuleta mabadiliko ya kweli nchini.
Mpina, ambaye awali alikuwa Mbunge wa Jimbo la Kisesa kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), alieleza kuwa alihama chama hicho baada ya jina lake kukatwa kwenye kura za maoni mwaka huu. Alidai kuwa hatua hiyo ilikuwa njama ya kuwapa nafasi mafisadi wa fedha za umma na kumwondoa bungeni kama mtoa hoja za msingi.
Katika kipindi chake cha uwakilishi, Mpina alitajwa kuwa chanzo cha maendeleo makubwa katika Jimbo la Kisesa. Alisimamia ujenzi wa barabara za kisasa, shule mpya 16 za sekondari, zahanati 15, na vituo viwili vya afya vinavyotoa huduma kamili. Pia alihusika katika uboreshaji wa miundombinu ya maji kutoka Ziwa Victoria na kampeni ya kuteketeza nyavu haramu.


