HABARI BANDIA ZAPEWA ONYO: WAANDISHI WATAHADHARISHWA KABLA YA UCHAGUZI 2025
![]() |
| katikati ni Jaji Mstaafu Robert Makaramba akiwa picha ya pamoja na wahariri na waandishi wa vyombo vya habari, 14 Agosti 2025, Millennium Tower - Dar es Salaam |
Na Kelvin Kijo, Dar es Salaam
Wahariri na waandishi wa habari nchini wametakiwa kuongeza umakini na uthibitisho wa taarifa wanazochapisha kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025, ili kuilinda demokrasia na kuepusha upotoshaji unaosababishwa na habari bandia zinazozalishwa kwa kutumia akili mnemba (AI).
Wito huo umetolewa kwenye mafunzo ya siku mbili yaliyofanyika jijini Dar es Salaam Agosti 14 na 15, 2025, chini ya uratibu wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), ambapo Meneja wa Programu, Josephat Mwanzi, alionya kuwa taarifa za uongo zinazotengenezwa mitandaoni zimekuwa zikitumika kuchafua taswira za watu na kuibua taharuki.
“Tunapaswa kuwa makini na maudhui tunayoyatoa. Vyumba vyetu vya habari vinahitaji nidhamu kubwa hasa kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu,” alisema Mwanzi.
Mkufunzi kutoka Nukta Afrika, Daniel Mwingira, alifafanua njia za kugundua taarifa na picha bandia zinazozalishwa na akili mnemba, akisisitiza umuhimu wa kuangalia chanzo cha habari, mazingira na muda wa kutolewa kwake. Pia alihimiza matumizi ya majukwaa ya uhakiki kama JamiiCheck kabla ya kusambaza taarifa zenye utata.
Kwa upande wake, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), William Shoo, alieleza kuwa zaidi ya Watanzania milioni 37 wamejiandikisha kupiga kura mwaka huu, huku asilimia 85 wakitegemea vyombo vya habari na mitandao kupata taarifa sahihi.
“Vyombo vya habari vinapaswa kuanza maandalizi angalau miezi mitatu kabla ya uchaguzi, vikizingatia mafunzo ya uthibitishaji taarifa, uandishi wa habari za data, na pia sheria za uchaguzi,” alisema Shoo.
Alikumbusha kuwa Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari ya mwaka 2016 na Kanuni zake za mwaka 2017 zinapaswa kuzingatiwa kwa umakini, akionya kuwa ukiukwaji wake unaweza kupelekea adhabu za faini au kifungo.
“Ni lazima tuhakikishe tunathibitisha vyanzo, tunawasiliana na wataalamu, na kurekebisha taarifa zisizo sahihi ndani ya saa mbili. Hivyo ndivyo tutakavyojenga imani ya umma,” alisisitiza Shoo.
Awali, Jaji Mstaafu Robert Makaramba, Mwenyekiti Kamati ya Maadili MCT, alizungumzia changamoto ya kuibuka kwa mamluki wa kidijiti wanaosambaza taarifa potofu, akisisitiza haja ya taifa kujenga tamaduni imara za pamoja katika kupambana na changamoto hii.


