Breaking News

DMI Yapiga Jeki Uchumi wa Buluu, Yaweka Mikakati Madhubuti

Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano), Abdallah Hassan Mitawi akisisiza dhamira ya serikali kuendeleza uchumi wa buluu

Na Kelvin Kijo

Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI) kimeahidi kushirikiana kikamilifu na Serikali kuhakikisha Tanzania inakuwa kitovu cha uchumi wa buluu katika ukanda wa Bahari ya Hindi.


Hayo yamebainishwa leo, Agosti 22, 2025 jijini Dar es Salaam, wakati wa maandalizi kuelekea uzinduzi wa Kongamano la Taifa la Wadau wa Uchumi wa Buluu litakalofanyika Septemba 10-11.


Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Makamu wa Rais, Mhe. Abdallah Hassan Mitawi, alisema serikali imejipanga kusimamia kikamilifu sera na fursa zinazotokana na rasilimali za majini ili kunufaisha Watanzania wote.


Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo cha Bahari (DMI), Prof. Tumaini Gurumo, alieleza kuwa ili sekta hiyo iwe na tija, ni lazima elimu na uwekezaji wa pamoja baina ya serikali na sekta binafsi vipewe kipaumbele.

Mkuu wa Chuo cha Bahari (DMI), Prof. Tumaini Gurumo (katikati) akieleza mikakati ya kukuza uchumi wa buluu 

“DMI imejipanga kuanzisha kozi maalum na mikakati madhubuti ya kusimamia uchumi wa buluu, ili sekta hii iwe chanzo cha pato la taifa, ajira na matumizi endelevu ya rasilimali maji,” alisema Prof. Gurumo.


Aidha, Prof. Gurumo alisisitiza umuhimu wa kuanzishwa kwa ofisi maalum ya kuratibu masuala ya uchumi wa buluu, jambo litakalosaidia katika sera na dira ya maendeleo ya 2050.

baadhi ya wajumbe wakiwa kwenye mkutano na waandishi wa habari kuelekea siku ya uzinduzi wa Kongamano la Uchumi wa Buluu, 10-11 September 2025