Breaking News

REA, STAMICO Kusaidia Mapinduzi ya Nishati Safi Kupitia Mradi wa Rafiki Briquettes Geita

Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) wamesaini mkataba wa ujenzi wa mtambo wa kuzalisha mkaa mbadala unaojulikana kama Rafiki Briquettes katika mkoa wa Geita, kwa kutumia vumbi la makaa ya mawe.

Na mwandishi wetu, Kelvin Kijo - Dar es Salaam

Mradi huu unalenga kulinda mazingira kwa kupunguza ukataji miti, kuongeza ajira na kipato, kupunguza hewa ya ukaa, na kuchangia utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa, hasa kuhusu afya, nishati safi, na mabadiliko ya tabianchi.

REA imechangia TSh bilioni 3 kugharamia ununuzi wa mtambo, huku STAMICO ikichangia TSh bilioni 1.58 kwa ajili ya eneo, ujenzi wa jengo la kiwanda na gharama za ufungaji mitambo. Huu ni mtambo wa tano kwa STAMICO, baada ya viwanda vilivyopo Kisarawe, Kiwira, Dar es Salaam (TIRDO), na viwili vinavyoendelea kukamilika Dodoma na Tabora.

Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Hassan Saidy, amesema Wakala unaendelea kushirikiana na wadau kuhakikisha upatikanaji wa nishati safi ya kupikia unafikia asilimia 80 ifikapo 2025, ikiwemo kupitia usambazaji wa majiko banifu, LPG, na gesi asilia.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO, Dkt. Venance Mwasse, amesisitiza kuwa STAMICO itaendelea kutekeleza maono ya Rais Samia Suluhu Hassan katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi, huku akieleza kuwa Rafiki Briquettes tayari inatumiwa na Magereza yote nchini, JWTZ, JKT, shule, vyuo, hoteli na migahawa.