Breaking News

MAKAMU WA RAIS PHILIP ISDOR MPANGO ATEMBELEA BANDA LA KAMPUNI YA MANSOOR INDUSTY

 Makamu wa Rais, Mhe.Dkt. Philip Isdor Mpango pamoja na Naibu Waziri Mkuu Mh. Doto Biteko wakipata maelezo kutoka kwa Altaf Hilan na Sajad Habib katika banda lao wakati wa  Kongamano na Maonesho ya Petroli ya Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAPCE’25) ambalo limefanyika   jijini Dar es Slaam.


Dar rs Salaamu

Makamu wa Rais, Mhe.Dkt. Philip Isdor Mpango amesema kuwa matumizi ya nishati katika Bara la  Afrika hasa Kusini mwa Jangwa la Sahara  bado ni madogo ikilinganishwa na maeneo mengine kama Bara la Amerika, Asia na Ulaya hivyo kuna umuhimu wa kubuni njia bora za kuzitumia rasilimali zilizopo ikiwemo Mafuta na Gesi Asilia ili kuwawezesha wananchi kustawi kiuchumi na kijamii huku suala la utunzaji wa mazingira likizingatiwa.

Amesema hayo tarehe 5 Machi, 2025 wakati akifungua rasmi Kongamano na Maonesho ya Petroli ya Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAPCE’25) ambalo litafanyika kwa muda wa Siku Tatu jijini Dar es Salaam.

“Katika kipindi ambacho maendeleo ya nishati endelevu yana mchango mkubwa katika mustakabali wa mazingira, uchumi na jamii zetu na katika kipindi ambacho Dunia inakabiliwa na changamoto za mabadiliko ya tabianchi bado tunahitaji  kutumia rasilimali zetu zilizopo, ikiwemo mafuta na gesi asilia lakini bila kuhatarisha mustakabali wa vizazi vijavyo ili kukidhi mahitaji ya kinishati.” Amesema Dkt. Mpango

Ameeleza kuwa, Afrika Mashariki imebarikiwa na rasilimali nyingi za nishati, ikiwemo mafuta na gesi asilia  ambapo  Tanzania imegundua gesi asilia, Uganda, Kenya na Sudan Kusini wamegundua mafuta, Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wana gesi ya methane, huku Kenya na Tanzania zikiwa na rasilimali za nishati jotoardhi hivyo rasilimali hizo lazima  zitumike ili kupunguza pengo la nishati na kuharakisha maendeleo.

“Tunatambua kuwa ulimwengu unakabiliwa na changamoto za mabadiliko ya tabianchi yanayosababisha madhara makubwa kama vile vipindi visivyotabirika vya mvua, mafuriko, mitetemeko ya ardhi na kuongezeka kwa joto. Tanzania, kama mataifa mengine, imejitolea kupunguza uzalishaji wa hewa ya ukaa  ili kupambana na mabadiliko ya tabianchi na kufanikisha azma ya kutozalisha hewa ya kaboni ifikapo mwaka 2050. Hata hivyo, tunapaswa kuweka uwiano kati ya ukuaji wa uchumi na uendelevu wa vyanzo vyetu  kwa kutatua changamoto za leo huku tukijiandaa kwa changamoto za kesho.” Amesema Dkt. Mpango