Maadhimisho ya Wiki ya Nenda kwa Usalama Zanzibar: NIT watoa mafunzo kwa madereva, makondakta
Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) kimetumia Maadhimisho ya Wiki ya Nenda kwa Usalama Barabarani visiwani Zanzibar kutoa mafunzo kwa madereva na makondakta wa mabasi ya abiria juu ya usalama barabarani, wakisema kuwaelimisha madereva na makondakta kuhusu kanuni za usalama barabarani na maadili mema ni muhimu sana katika jitihada za kupunguza ajali za barabarani nchini.
Hayo yamebainishwa na wataalamu kutoka Chuo cha Taifa cha Usafirishaji ambapo waliongea katika semina kuhusu ‘Kanuni za Usalama Barabarani’ kwa madereva na makondakta wa vyombo vya usafiri wa umma katika kuadhimisha ‘Wiki ya Usalama Barabarani mwaka huu iliyoanza Novemba 12 hadi 23, mwaka huu.
Bw Godlisten Msumanje, Mkuu wa Kituo cha Umaahili cha Usalama barabarani cha Kikanda wa NIT amewataka madereva na makondakta nchini, kwenda mara kwa mara kupata mafunzo ili kuwa ‘madereva wa kutegemewa'.
“NIT iliamua kushirikiana na Mamlaka ya Usalama Barabarani Zanzibar (ZARSTA) kuwakumbusha madereva na makondakta kuhusu sheria, kanuni na maadili ya barabarani kwa sababu wengi wanazisahau, huku wengine wakipuuza tu au hawana mawazo ya kuendelea kuongeza ujuzi baada ya kupata leseni. ,” Msumanje alieleza.
Alisisitiza kuwa madereva na makondakta wanatakiwa waendelee kupata mafunzo ya usalama barabarani ili waendele kuzingatia utekelezaji kwa vitendo.
Naye Mhandisi Mhoja Luhende Mahoha kutoka NIT alisema kuwa asilimia themanini ya ajali za barabarani ni matokeo ya makosa ya kibinadamu, na pia ubovu wa magari unachangia, “Kwa hiyo ni wajibu wa madereva kufuata kanuni na kuhakikisha mnaendesha magari vizuri.”
Pia alisema makondakta wanatakiwa kuelimishwa upya juu ya umuhimu wa kuwatendea heshima abiria au wasafiri wao wakiwemo watoto wa shule, na kuwa wasafi wakati wa saa za kazi.
Wawezeshaji hao kutoka NIT pia waliwataka wasimamizi wa sheria kutekeleza wajibu wao, kuwakumbusha madereva na makondakta wote juu ya kuzingatia kanuni za barabarani ili kupunguza ajali za barabarani Zanzibar.
Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani (RTO) Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP) Hamis Mwakanolo pamoja na Bw. Bilali Salum Said- Mwenyekiti wa Taifa wa Jumuiya ya Skuli za Udereva Zanzibar wameungana na watoa mada kutoka NIT wakisema mafunzo endelevu ni muhimu kwa madereva na makondakta kwani yanawasaidia kuwakumbusha kanuni na taratibu za usalama barabarani.
"Bado tunaweza kupunguza ajali za barabarani ambazo zinazoweza kuepukika kutokana na uzembe," ASP Hamis alisema huku Bilali akieleza kuwa uzembe miongoni mwa madereva daima husababisha ajali.




