Breaking News

TANZANIA YA ZALISHA BIDHAA BORA ZA NGOZI

 


Na Wellu Mtaki, Dodoma

Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), Bw.I Fortunatus Makore Magambo, amesema Tanzania ina uwezo mkubwa wa kuzalisha bidhaa bora za ngozi zinazoweza kushindana katika soko la kikanda na kimataifa kutokana na upatikanaji wa malighafi za kutosha pamoja na uwekezaji uliofanyika katika sekta hiyo.

Magambo alitoa kauli hiyo katika Ukumbi wa Msekwa, Bungeni jijini Dodoma, alipokuwa akiwasilisha taarifa ya shughuli na mafanikio ya Kiwanda cha Ngozi cha Kilimanjaro (Kilimanjaro International Leather Industries Company Limited - KLICL). Katika wasilisho lake, aliwataka Waheshimiwa Wabunge kuwa mabalozi wa bidhaa za ngozi zinazozalishwa nchini kwa kuzitumia na kuzitangaza ili kusaidia kukuza viwanda vya ndani, kuongeza ajira na kuimarisha uchumi wa taifa.

Alisema KLICL imeendelea kuwa miongoni mwa viwanda vikubwa vya uchakataji wa ngozi nchini, kikizalisha bidhaa mbalimbali zikiwemo viatu, mikanda, mabegi na bidhaa nyingine zinazokidhi viwango vya ubora vya kimataifa.

“Tunawaomba Waheshimiwa Wabunge muwe mabalozi wa bidhaa za ngozi zinazozalishwa hapa nchini. Mkitumia na kuzitangaza, mtasaidia kujenga imani kwa wananchi na kuongeza soko la bidhaa zetu za ndani,” amesema Magambo.

Ameeleza kuwa kuongezeka kwa matumizi ya bidhaa zinazozalishwa nchini kutasaidia kuongeza thamani ya mazao ya mifugo, kuchochea ukuaji wa sekta ya viwanda, kuongeza ajira kwa vijana na kuimarisha mapato ya fedha za kigeni kupitia mauzo ya bidhaa hizo katika masoko ya nje.

Kwa mujibu wa Magambo, KLICL inaendelea kutekeleza mkakati wa kupanua masoko ya bidhaa zake ndani na nje ya nchi ili kuhakikisha uwezo wake mkubwa wa uzalishaji unatumika kikamilifu. Alitaja masoko yanayolengwa kuwa ni pamoja na nchi za Afrika Mashariki pamoja na mataifa ya China, Saudi Arabia, Italia, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), Misri, Pakistan na Uturuki.

Katika hatua inayoashiria kuongezeka kwa ushindani wa bidhaa za ngozi za Tanzania katika soko la kimataifa, menejimenti ya KLICL imeeleza kuwa wanunuzi kutoka China tayari wameidhinisha sampuli za bidhaa zake, jambo linalotarajiwa kufungua fursa za oda kubwa zaidi siku zijazo.

Aidha, kiwanda hicho kimefanikiwa kuuza vipande 48 vya ngozi ya mbuzi kwenda China kwa thamani ya dola za Marekani 15,000, hatua inayotajwa kuwa ishara ya kuongezeka kwa mahitaji ya bidhaa za ngozi zinazozalishwa nchini katika masoko ya kimataifa.

Pamoja na mafanikio hayo, Magambo amesema changamoto kubwa inayolikabili kwa sasa ni upanuzi wa masoko ili kuendana na uwezo wa uzalishaji wa kiwanda hicho. Alisisitiza kuwa ushirikiano wa viongozi, sekta binafsi na wananchi katika kuhamasisha matumizi ya bidhaa za ndani ni muhimu katika kufanikisha azma ya Tanzania ya kujenga uchumi wa viwanda.

KLICL ni miongoni mwa viwanda vikubwa na vya kisasa zaidi vya uchakataji wa ngozi katika Afrika Mashariki na Kati. Kikiwa na teknolojia ya kisasa, kiwanda hicho kina uwezo wa kuzalisha bidhaa bora, imara na zinazokidhi viwango vya kimataifa.

Kupitia uwekezaji huo, Tanzania inaendelea kuongeza thamani ya rasilimali zake na kuifanya sekta ya ngozi kuwa miongoni mwa nguzo muhimu za maendeleo ya viwanda na ukuaji wa uchumi wa taifa.